Miaka 50 ya BOT na mafanikio ya kiuchumi - MUANGALIZI

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, June 14, 2016

Miaka 50 ya BOT na mafanikio ya kiuchumi

Benki kuu ya Tanzania

Miongoni mwa majukumu ya  Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ni kusimamia kikamilifu masuala mbalimbali ya kibenki na kifedha ikiwemo  masoko ya fedha za kigeni, mifumo ya malipo yote ni kuhakikisha uchumi nchi unakuwa na kuwa na manufaa kwa kila mtanzania.

Kwa mujibu kutoka benki hiyo inaeleza kuwa  Juni 14 mwaka huu  BOT inasherekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kama Benki Kuu ya Taifa.
 Benki kuu  ilianzishwa kwa sheria ya mwaka 1965 (The Bank of Tanzania Act 1965) na ilianza kufanya kazi rasimi14 Juni mwaka 1966. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo  majukumu na shughuli za Benki Kuu na muundo wake umekuwa ukibadilika kulingana na mabadiliko  ya sera za kijamii na kiuchumi nchini pamoja  na maendeleo ya kiuchumi na mfumo wa fedha kikanda na kimataifa. 

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1967 hadi 1991, BOT ilijikita zaidi kufanikisha juhudi za Serikali katika kutimiza malengo ya kukuza uchumi katika mlengo wa ujamaa na kujitegemea.
Kwa wakati huo sera ya fedha ilitegemea maelekezo kutoka Serikali Kuu ambapo Sera ya fedha ilikuwa ikitekelezwa kwa kutumia miongozo ya fedha na mikopo na ile ya fedha za kigeni  sambamba na udhibiti katika riba na upatikanaji wa mikopo na fedha za kigeni. 

Hata hivyo  hali hiyo, ilipelekea kudhoofu kwa mihimili mikuu ya uchumi  sambamba na ongezeko kubwa la ujazi wa fedha, mfumuko wa bei, kuporomoka kwa thamani ya Shilingi na kudhoofu kwa kasi ya ukuaji wa uchumi.

Aidha taarifa hiyo inaeleza kwamba kutokana na udhaifu huo uliojitokeza, Serikali ilichukua hatua za makusudi kuunusuru uchumi mwishoni mwa miaka ya 1980,  kwani mwaka 1986 juhudi mbalimbali zilifanyika  katika kuendeleza shughuli  za kufufua uchumi.


Mwaka 1988 moja ya hatua serikali ilizochukua ilikuwa ni  kuunda Tume ya Uchunguzi chini ya Gavana Charles Nyirabu ili kushughulikia matatizo katika sekta ya fedha.
 Kwa kuzingatia mapendekezo ya tume hiyo, iliundwa Sheria ya benki na Taasisi za fedha ya mwaka 1991 (Banking and Financial Institutions Act) kufungua njia kwa sekta binafsi kushiriki katika kuendeleza sekta ya fedha.


Sanjari na hayo sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1995 (Bank of Tanzania Act) ilitungwa na kuiwezesha BOT kuondokana na majukumu mengi na kujikita katika jukumu moja kuu la usimamizi wa utulivu wa bei.
Mabadiliko haya ambayo yalikuwa na malengo mazuri ya kukuza uchumi na kuwa na faida katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na kulisaidia taifa la tanzania kusonga mbele katika uchumi.
Baada ya mabadiliko mafanikio katika utekelezaji wa sera mbalimbali,
 hususan, sera ya fedha kama inavyojionyesha katika kushuka kwa kasi 
ya mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka benki kuu mfumuko wa bei ulipungua
 kutoka wastani wa asilimia 30 katika miaka ya 1980 hadi chini ya asi
limia 10 kwa miaka ya hivi karibuni ambapo, ukuaji halisi wa uchumi 
umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa asilimia 7 katika kipindi cha m
uongo mmoja na nusu uliopita, sambamba na ongezeko la mikopo kwa
 sekta binafsi.

Aidha upatikanaji wa huduma za kifedha umeongezeka  na kufikia 
asilimia 79 ya idadi ya watu wazima hapa nchini wanapata huduma 
rasmi za kifedha katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania, kazi kuu ya benki nchini Tanzania (wakati huo Tanganyika) ilifanywa na mashirika mbalimbali.
Mathalani kampuni ya Kijerumani ya Afrika Mashariki (Germany East African Company) ambayo ilikuwa inasimamia koloni la Kijerumani la Afrika Mashariki ndiyo iliyokuwa na wajibu wa kudhibiti ujazi wa fedha mpaka mwaka 1903.

 Wakati huo, Benki itwayo Deutsch-Ostafrikanische Gesellschaft ilipewa jukumu la kuchapisha sarafu zilizoanza kutumika Tanganyika mwaka 1905.

Jukumu hilo baadaye lilichukuliwa na Serikali ya Ujerumani mpaka mwaka 1918 na sarafu iliyokuwa inatumika wakati huo ilikuwa inaitwa Rupia
.
Taarifa kutoka BOT inaeleza kuwa kwa upande wa Zanzibar, jukumu la fedha lilikuwa chini ya Utawala wa Uingereza,ambapo jukumu la kusimamia ujazi wa fedha lilisimamiwa na serikali ya Uingereza.

Hivyo kipindi cha pili ni baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-18), ambapo Uingereza ilitawala Tanganyika na Zanzibar, mfumo wa malipo uliokuwa unatumika wa fedha taslimu na hundi zilizotolewa na mfumo wa benki za kikoloni ambao ulishamiri hasa kwenye miji mikubwa.
Mwaka 1919 sarafu ya Afrika Mashariki ilianzishwa  kwa ajili kudhibiti ujazi wa fedha katika makoloni ya Uingereza ya Afrika Mashariki na nchi jirani.

 Mwaka 1921 sarafu ya Rupia iliondolewa na kuanzishwa mfumo wa Poundi pamoja na Shilingi.
Taarifa hiyo ya benki inaeleza kuwa  historia ya Sera ya Fedha Tanzania ilianza mwaka 1919 wakati Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ilipoanzishwa kwa lengo la kusimamia ujazi wa fedha katika nchi za Kenya, Uganda na Tanganyika. 

Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ilikuwa mtazamaji wa fedha na hasara yake ilikuwa kutokuwa na uwezo wa kusimamia sera ya fedha. 

Tangu kuanzishwa kwa BOT, sera ya fedha nchini imekuwa ikibadilika mara kwa mara kwani katika kipindi cha mwaka 1960 hadi 1970, sera ya fedha ya Benki Kuu ilitegemea maelekezo kutoka serikali Kuu kupitia miongozo ya fedha na mikopo na ile ya fedha za kigeni iliyoanzishwa mwaka wa 1971/72.  

Mipango ya matumizi ya fedha za kigeni iliandaliwa kulingana na vipaumbele vya taifa. Sera ya fedha ya BOT ilitegemea zaidi maelekezo kutoka serikalini. Katika kipindi hicho hakukuwa na soko la mitaji wala la fedha.

 Aidha zana ya fedha pekee iliyokuwepo ni dhamana za Serikali ambazo zilitolewa kwa kampuni ya Bima ya Taifa, mifuko ya hifadhi ya Jamii na Benki ya Posta. Benki zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali ndizo zilitawala mfumo wa kibenki na riba ilikuwa inapangwa na utawala.

Udhibiti huo wa moja kwa moja ulionekana kuwa ni chanzo kimojawapo cha matatizo ya uchumi yaliyotokea mwanzoni mwa miaka ya 1980 kutokana na kuwa na thamani kubwa kuliko uhalisia wake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot