Mh. Edward ngoyai Lowassa |
Kwa mujibu wa waraka huo, Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisema amelazimika kufikisha ujumbe huo kwa IGM Mangu kutokana na mambo mazito yanayoweza kuathiri mustakabali mwema wa kitaifa.
Alisema msingi wa waraka huo ni agizo ulilotoa IGP Mangu juu ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa, maandamano ya vyama vya upinzani.
"Wakati IGP Mangu akitoa agizo hilo, mimi nilikuwa nje ya nchi ingawa Watanzania wenye mapenzi mema na Taifa lao waliopo nchini na nje, walinifikishia taarifa za agilo lako.
"Niwie radhi kwa kukiuka taratibu za kiitifaki, nimelazimika kwa nafasi yako na yangu, kuandika waraka huu kwako...si desturi yangu kuandika waraka wa namna hii mtandaoni au kupitia vyombo vya habari ingawa safari hii nimelazimika kufanya hivyo ili kuweka rekodi sahihi na kukosoa sababu ulizotoa," alisema Lowassa katika waraka huo.
Lowassa aliongeza kuwa, wakati akitafakari kwa mshangao agizo hilo na baada ya kurejea nyumbani, alipigwa na butwaa aliposikia jeshi hilo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, liliwazuia viongozi wa chama hicho ngazi ya Taifa kufanya mikutano ya hadhara.
Aliongeza kuwa, agizo hilo lilifuatiwa na tukio la kukamatwa, kushikiliwa na kuhojiwa kwa viongozi hao akiwamo Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, jijini Mwanza.
"Katika matukio hayo, polisi mnadai kuwa na taarifa za kiintelijensia ambazo zinazonesha kuwapo uwezekano wa kutokea kwa vurugu kwenye mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
"Kwa mujibu wa madai haya, hata wewe binafsi (IGP Mangu), umepata kuyatoa awali ulipoamua kwa sababu mnazojua ninyi kuminya haki za msingi na kikatiba za vyama vya siasa kujumuika, kutimiza majukumu yao ya kisiasa ambayo hayana ukweli hata kidogo," alisema.
Alisema uzoefu wa kihistoria unakinzana, kwenda kinyume kabisa na madai hayo kwani yako matukio mengi ambayo yamethibitisha kuwa, mijumuiko ya wanasiasa wa vyama vya upinzani yakiwamo maandamano, mikutano imekuwa ikifanyika kwa amani.
Katika waraka huo, Lowassa alifafanua kuwa, iko mifano mingi inayoonesha kwamba wapinzani wamefanya shughuli mbalimbali za kisiasa kwa maana ya maandamano, mikutano ya hadhara
kwa amani pasipo kuwapo ulinzi wa polisi.
Alisisitiza kuwa, mifano ya namna hiyo ndiyo inayowafanya wapingane na maagizo yanayotoa mwelekeo wa kukandamizwa uhuru wa kikatiba wa vyama vya upinzani kujumuika ya kuyatilia shaka wakiamini ni misukumo iliyojificha nyuma ya kichaka cha 'sababu za kiintelejensia'.
"Naandika waraka huu kwako nikiamini kwa dhati kuwa, kilichotokea nchini Kenya hivi karibuni ambako mahakama ilitupilia mbali maagizo ya namna hii yaliyotolewa na polisi waliokuwa wakijaribu kuzuia haki ya kikatiba ya vyama vya upinzani kuandamana, ndicho kinachoelekea kutokea nchini kwetu.
"Si hilo tu, naamini wewe IGP ulifuatilia kile kilichotokea nchini Uganda siku chache baada ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda kutangazwa mshindi wa nafasi ya urais, chama kimoja cha siasa kiliitisha mkutano wa hadhara na kikamwapisha Kizza Besigye ambaye wao wanaamini ndiye aliyeshinda urais," alisisitiza Lowassa katika wakara huo.
Aliongeza kuwa, Waganda ambao wamekuwa wakiiamini mgombea wanayemuunga mkono ndiye aliyeshinda japo kura zake ziliibwa, waliruhusiwa kuandamana, kukutana kwa uhuru ingawa baadaye walikamatwa hivyo hilo ni jambo la kujifunza kwamba Waganda hawakuzuiwa na uwepo wa taarifa za kiinteligensia licha ya kukamatwa na kushtakiwa baadae.
Alisema wapinzani wanajifunza kuwa, mamlaka za dola kama lilivyo Jeshi la Polisi, linapaswa kuheshimu, kulinda haki za raia, kuepuka hatari ya vyombo hivyo kujipa dhamana ya kuwaamulia wananchi masuala yao kwa kisingizio cha taarifa za kiintelijinsia.
Katika waraka huo, Lowassa alikwenda mbali zaidi na kuhoji; "Je, kwa maagizo ya namna hii, IGP Mangu na wenzako polisi mnatuonaje sisi viongozi wa upinzani...Je, mnafikiri pamoja na uzoefu wetu katika siasa na uongozi tunaweza tukawa mbumbumbu wa kutambua haki zetu au kushindwa kujua dhamana kubwa tuliyobeba
ya kuwatumikia wananchi na Taifa letu?
"Je, IGP Mangu na wakuu wenzako wa Jeshi la Polisi mnapotoa maagizo ya namna hii hamuoni kwamba mnajenga taswira tu kwamba malengo yenu ni kutafuta jinsi ya kutumia magari ya upupu yaliyoagizwa kwa pesa nyingi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana?
Aliongeza kuwa; "Je, mmeshindwa kujifunza kwamba kama kulikuwa hakuna vurugu kabla, baada ya Uchaguzi Mkuu mbali ya kuwapo kila viashiria vilivyochochewa na taasisi za dola, wapinzani hatuna sababu hata moja ya kuwa chanzo cha vurugu za namna hiyo?
Alisema pengine ni busara akakumbusha kwamba, vyama vya upinzani chini ya mwavuli wa UKAWA, viliwahi kuandamana kwa maelfu kutoka Buguruni yaliko Makao Makuu ya CUF hadi Makao Makuu ya CHADEMA Kinondoni kwa amani na utulivu.
"Je, hukumbuki kwamba katika maandamano hayo yaliyohusisha maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam, hakuna sindano ya wmananchi iliyopotea wala mtu kukwaruzwa...hayo na mengine mengi ndiyo yaliyonifanya nitafakari sana na kukosa jibu ninaposikia polisi mkituzuia kwenda
vijijini kuwashukuru wananchi waliotuheshimu, kutupiga kura.
"Nini ambacho kitaathiri amani na utulivu...wanachama wa vyama vipi ambao eti watapingana kwa sababu sisi tumeamua kuwashukuru wananchi waliotuunga mkono kwa mamilioni, nakuomba IGP Mangu uyatafakari haya na kuliangalia upya agizo lako ambalo yamkini haliitakii mema nchi yetu," ulisisitiza waraka huo.
Zuio la Polisi
Juni 7, mwaka huu, Jeshi la Polisi lilitoa tamko la kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia siku ya tamko hadi hali ya usalama itakapotengemaa.
Tamko hilo lilitolewa na Kamishina wa Polisi Operesheni na Mafunzo,kutoka Makao makuu ya Polisi, CP Nsato Mssanzya, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema hivi karibuni, jeshi hilo limepokea taarifa za baadhi ya vyama vya siasa kutaka kufanya mikutano, maandamano lakini kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya habari, wamebaini mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi (Civil disorder).
CP Mssanzya aliongeza kuwa, vyama vingine vya siasa vimeonesha dhamira ya kupinga kile ambacho kitasemwa na wapinzani wao pia upo uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu kati ya makundi mawili ya kisiasa.
"Kwa hali hiyo, tunapiga marufuku maandamano, mikutano ya hadhara kuanzia leo Julai 7, mwaka huu hadi hali ya usalama itakapotengemaa, tunawataka wanasiasa kuacha mara moja kushinikiza wananchi kutotii sheria za nchi kwani hatutasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote, chama cha siasa kitakachokaidi agizo hili," alisema.
Aliwataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wenye lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi badala yake linawasihi waendelee kushirikiana katika kujenga umoja wa nchi.
Mbowe, wenzake wakamatwa
Juni 12, mwaka huu, Mwenyekiti wa CHADEMA (Mbowe), alikamatwa na Jeshi la Polisi mkaoni Mwanza, kuhojiwa kwa saa mbili katika Kituo cha Polisi cha Nyakato, wilayani Nyamagana.
Msemaji wa CHADEMA, Tumaini Makene, alisema mbali na Mbowe, baadhi ya viongozi wengine waliokamatwa ni Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka na Katibu Mkuu 'BAVICHA', Julius Mwita.
Akizungumza baada ya kuhojiwa na polisi, Mbowe alisema alitakiwa kutulia kwenye hoteli aliyofikia, asitoke kwenda mahali popote jijini humo bila kuwataarifu polisi, masharti ambayo aliyakataa.
"Polisi wamenitaka nisitoke hoteli niliyofikia bila kutoa taarifa kwao,
hili nimelikataa maana huku ni kunipa kifungo cha nje kama kiongozi
wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye.
"Nimewajibu mimi ni kiongozi wa Taifa kama wa CCM, nina haki
ya kutembelea ofisi zangu pia kama Mtanzania nina haki ya
kutembea popote,” Mbowe anakaririwa.
Mbowe alikamatwa na polisi wakati akitembelea matawi mbalimbali
ya chama hicho jijini humo na ofisi za chama.
No comments:
Post a Comment