KAMA kuna waziri au kiongozi yeyote
anataka kutoa taarifa yenye kuwagusa wananchi moja kwa moja, ni dhahiri
kuwa sasa atalazimika kujiridhisha zaidi.
Aidha, waziri na viongozi wengine
wanatakiwa pia kuzingatia dhana ya uongozi wa pamoja kwa kuwahusisha
wenzao na pia kupata maoni ya wataalamu katika wizara au taasisi
wanazoziongoza kabla ya kulifikisha kwa umma.
Vinginevyo, mawaziri wajiandae
kushuhudia maagizo yao yakitenguliwa huku pia wakijiweka katika hatari
ya kufikiriwa kuwa wanafanya hivyo kwa minajili ya kutumia matamko yao
kama ‘kiki’ za kuwaonyesha kuwa wanafanya kazi vyema na kwa kasi
inayosisitizwa na Serikali ya awamu ya tano.
Angalizo hilo limetolewa na baadhi ya
wachambuzi wa amsuala ya kisiasa walizoungumza na Nipashe kuelezea mkasa
uliomkuta Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye
agizo lake la kuzuia ufungishaji ndoa kwa watu wote wasiokuwa na vyeti
vya kuzaliwa lilifutwa na Rais John Magufuli kwa kuonekana kuwa
litawaathiri mamilioni ya Watanzania wasiokuwa na vyeti hivyo.
Baadhi ya wachambuzi walidai kuwa
Mwakyembe siyo waziri au kiongozi wa kwanza kutoa taarifa zilizomlazimu
Rais Magufuli kuingilia kati kwa manufaa ya Watanzania na hivyo,
wanapaswa kujua kuwa wana wajibu mkubwa kwa taifa na kutakiwa wajiepushe
na matamko binafsi yasiyofanyiwa kazi kwa kina kabla ya kutolewa kwa
umma.
“Ni vizuri kwa kila waziri au kiongozi
yeyote yule kujipa uhakika wa kila tamko na amri wanazotaka kutoa kwa
umma…kwa mfano, ni lazima wahakikishe kwamba wanazingatia sheria na pia
wanayoyasema ni kwa maslahi ya umma mpana wa Tanzania.
“Vinginevyo, matamko yao yataendelea
kuibua maswali na Rais hatakubali wamharibie kwa sababu ameshasema mara
kadhaa kuwa daima atakuwa upande wenye maslahi kwa wananchi wake, na
hasa wanyonge,” alisema mmoja wa wachambuzi hao.
“Ni vizuri wakaachana na matamko yenye
viashiria vya kuwa na kiki za kuonyesha kuwa nao wako vizuri kuendana na
kasi ya serikali ya sasa...wasipozingatia hayo kila mara watajikuta
wakiwa tofauti,” mwingine aliongeza.
Neno ‘kiki’ ni la mtaani na limejitwalia
umaarufu katika siku za hivi karibuni, likitumiwa kumaanisha mbinu
zinazoweza kutumiwa na mtu ili kujipatia umaarufu juu ya jambo fulani.
Wasanii na wanasiasa huhusishwa zaidi na neno hilo kutokana na asili ya
kazi zao ambazo huwakutanisha zaidi na watu.
Awali, katika agizo lake hilo ambalo
alilisisitiza pia jana asubuhi wakati akizungumza na kituo kimoja cha
redio jijini Dar es Salaam, Mwakyembe alisema wameamua kuzuia ndoa kwa
watu wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa kwa nia ya kuondokana na takwimu za
sasa zinazoonyesha kuwa Tanzania Bara ni ya mwisho barani kwa utoaji wa
vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi wake.
Alisema ni asilimia 12 tu ya Watanzania
walioko Bara ndiyo wenye vyeti vya kuzaliwa na kuzidiwa hata na Zanzibar
yenye wastani wa asilimia 75, hali aliyosema inashangaza kwa sababu bei
ya vyeti hivyo ni Sh. 3,500 tu huku gharama za harusi zikiwa kubwa
kulinganisha na kiasi hicho.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa
habari muda mfupi kabla ya kuondoka mjini Dodoma na baadaye taarifa yake
kusambazwa kwa umma jana, Rais Magufuli alisema anatengua uamuzi huo wa
Waziri Mwakyembe kwa sababu utawanyima fursa ya kuoana Watanzania ambao
wengi wao hawana vyeti hivyo vya kuzaliwa, hasa wale wa vijijini.
Alisema hadi sasa idadi ya Watanzania
walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20 huku wengi wao
wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo,
na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya
kuzaliwa nchini mwaka 1961.
“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania msiwe
na wasiwasi wowote, endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama
kawaida na kama kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu
awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Harrison Mwakyembe apeleke Bungeni kikarekebishwe”
alisema Rais Magufuli, huku akitoa wito kwa wanasheria kuziangalia
vizuri sheria zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili
zisilete mkanganyiko kwa wananchi.
JPM ALIVYOZIMA ‘KIKI’
Mbali na tukio la kuzimwa kwa ‘kiki’ ya
Waziri Mwkayembe jana, wapo pia mawaziri na viongozi wengine kadhaa wa
serikali na taasisi za umma waliokumbana na rungu la Magufuli la
kutengua amri au tarifa zao. Hao ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista
Mhagama; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Mhagama alikumbana na mkasa huo Machi 3,
2016 wakati alipotoa taarifa ya kumteua Dk. Carina Wangwe kuwa Kaimu
Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Hata hivyo,
wakati uamuzi wake ukimpa umaarufu siku hiyo kupitia ‘kiki’ za kwenye
mitandao ya kijamii, waziri huyo alilazimika kubatilisha taarifa hiyo
kabla Rais Magufuli hajamtangaza Prof. Godius Kahyarara kushika nafasi
hiyo NSSF.
Agosti 12 mwaka jana, Simbachwene
alisisitiza kuondolewa kwa wamachinga maeneo ya mijini. Hata hivyo, siku
chache baadaye, Magufuli alitengua agizo hilo wakati akihutubia jijini
Mwanza kwa kutaka wamachinga wasiondolewe kwenye maeneo wanayofanyia
biashara hadi pale mamlaka husika zitakapohakikisha kuwa zimewatafutia
sehemu za kwenda kufanyia biashara zao.
Waziri mwingine aliyekumbwa na rungu la
Magufuli hivi karibuni wakati kauli yake ikiwa imepamba moto na kuibua
mijadala kwenye mitandao ya kijamii ni Nape.
Machi Mosi mwaka huu, Nape alielezea
umuhimu wa kulinda majina ya wasanii waliotajwa hadharani wakituhumiwa
kuhusika na dawa za kulevya, akisema kwamba ni vyema kuzingatia nguvu
kubwa walizotumia kujijengea majina hayo na kwamba, ifikiriwe pia ni kwa
namna gani watasafishwa ikiwa wataonekana baadaye kuwa hawahusiki na
dawa za kulevya.
Nape alizungumza hayo akiwa Dodoma na
baadaye kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV kuelezea hatua
iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,
aliyetangaza hadharani majina ya wasanii kadhaa katika orodha yake ya
awali ya watuhumiwa 65 wa dawa za kulevya.
Hata hivyo, siku chache baadaye,
Magufuli alionekana kupinga maelezo ya Nape kwa kusisitiza kuwa vita
dhidi ya dawa za kulevya isiangalie majina ya watu kwa sababu athari
zake ni kubwa kwa taifa.
WALICHOSEMA WABUNGE, WASOMI WANENA
Akizungumzia suala la Mwakyembe, Mbunge
wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), alisema ni ishara kuwa baadhi ya
mawaziri na viongozi wengine wamekuwa wakikurupuka kwa kutoa matamko
bila kuyafanyia utafiti wa kina na ndiyo maana Magufuli ametengua agizo
alilotoa kuhusu amri ya kuzuia ndoa kwa wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni
(CCM), alisema awali alikuwa haamini na mwishowe akajikuta akisikitika
kusikia tamko la Waziri Mwakyembe kuhusu zuio la ndoa kwa wasiokuwa na
vyeti vya kuzaliwa kwa sababu agizo lake halikuwa na msingi wa kisheria.
Alisema kupitia mkasa huo wa Mwakyembe,
mawaziri wanatakiwa kuwa makini katika kutoa matamko ya aina hiyo na
kwamba, kama wana hoja wanatakiwa kupeleka ndani ya Bunge ili ijadiliwe.
“Kama unatoa tamko leo na Rais
analipinga ama kulifuta, hiyo inaonyesha kuwa waziri umekurupuka…
matamko kama haya yanamgombanisha Rais na wananchi wake. Mawaziri
wajiepusha kutoa matamko ambayo hayajapewa ridhaa,” alisema Chegeni.
Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein
Bashe, alisema alichokifanya Rais Magufuli kutengua tamko hilo yupo
sahihi kwa kuwa suala la ndoa linagusa imani ya mtu na serikali
haitakiwi kuingilia, na kwamba kama kuna jambo la kisheria liwasilishwe
bungeni ili lifanyiwe kazi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk. Richard Mbunda, alisema inavyoonekana, huenda tangazo
alilitoa Mwakyembe ni binafsi kwa mtazamo wake baada ya kuona kuna
udanganyifu mkubwa katika eneo hilo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki
za Bindamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema agizo la Mwakyembe
kuhusu masuala ya ndoa linashangaza kwa sababu halipo kwa mujibu wa
sheria
“Katika Sheria ya Ndoa, vitu ambavyo mtu
anatakiwa kuwa navyo ili afunge ndoa ama sifa, hiyo ya cheti (cha
kuzaliwa) haipo… sijui huyo Waziri ameitoa wapi na pia ingekuwepo
kisheria ingepingwa kwa sababu watu wengi hawana vyeti vya kuzaliwa,”
alisema Bisimba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk. Ally Bashiru, alisema ni vyema Rais Magufuli ameingilia na
kutengua agizo la Mwakyembe la kuzuia ndoa kwa asiokuwa na vyeti vya
kuzaliwa.
No comments:
Post a Comment