Wacheza Karate nchini watahadharisha - MUANGALIZI

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Saturday, November 26, 2016

Wacheza Karate nchini watahadharisha


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, Picha na Maktaba.
MKUU wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva amewataka vijana wenye taaluma ya karate nchini kuyatumia vyema mafunzo hayo katika kujihami na kulinda usalama wa Ttaifa badala ya kujikita katika kutenda vitendo vibaya vinavyopelekea uvunjifu wa amani.

Akizungumza na Wadau mbalimbali waliojitokeza kuchangia damu katika viwanja vya Mwembe Yanga Temeke jana, Lyaniva amesema vijana hao wanapaswa kuitumia vyema taaluma hiyo na kuacha kujiingiza kwenye makundi mabaya ikiwemo Panya Road ambao wamekuwa wakihatarisha usalama wa raia pamoja na mali zao.

"Nimeona mambo mazuri yaliyooneshwa na hawa vijana wetu wa karate na ni imani yangu watatumia taaluma waliyonayo katika kuhakikisha ulinzi wetu unaimarika lakini kama watakuwa wanatumia vibaya nguvu zao nahakika hawataweza kuishi kwa muda mrefu kwa kuwa sasa hivi Serikali hatutaki kuona mambo ya uhalifu yakiendelea zaidi," alisema Lyaniva.

Amesema wataalamu wa karate ndio watu wanaotegemewa katika kuimarisha ulinzi lakini wao wamekuwa ndio watu wa kwanza katika kufanya vitu visivyopendeza kwa kuwatendea wasio na nguvu vitendo vya kinyama vyenye dalili zote za uzalilishaji.

Katika hatua nyingine Lyaniva amewaahidi waendesha baiskeli wa jumuiya hiyo kuwafungulia akaunti kila mmoja wao katika benki ya Amana ili kuwawezesha kufanikisha safari yao ya kwenda nchini Saudi Arabia ambako walipanga kutumia usafiri huo kutoka Tanzania mpaka Maka ambako ndio huenda kuhiji.

Amesema anatambua umuhimu wa waendesha baiskeli hao na yeye kama kiongozi wa Serikali ameguswa na madereva hao na kuahidi kushughulikia akaunti zao ili waweze kupatiwa mikopo isiyo na riba itakayowasaidia kwa kupata nauli pamoja na fedha za mahitaji mengine watakayoyahitaji pindi watakapokuwa huko nchini Saudi Arabia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa waendesha Baiskeli wa JAI, Ibrahim Minja amesema wameamua kufanya matembezi ya baiskeli katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuweza kuwahamasisha watu kujitokeza katika kuchangia damu na kumaliza tatizo hilo ambalo linaonekana kuumiza serikali kwa sasa.

Amesema Matembezi hayo yamehusisha zaidi ya madereva 18 kutoka mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Tanga, Moshi pamoja na Lindi na kushirikisha waendesha baiskeli wenye umri tofauti tofauti huku wengi wao wakiwa ni watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 40.

Akizungumzia msaada walioupata kutoka kwa Mkuu wa wilaya, Minja amesema kuwa wanayofuraha ya kumpata kiongozi ambae amekuwa makini na kutambua mahitaji ya wananchi kwa wakati jambo linaloongeza utayari kwa wao kufanya kazi nzuri zaidi ya hiyo waliyoifanya.

"Kwa mambo haya ambayo Lyaniva ametufanyia tunaahidi kuhamasisha zaidi watu wengi katika kuchangia damu ili tuweze kwenda kumaliza matatizo yanazisumbua hospitali zetu kwa sasa hasa kwenye hili janga la damu kwani tunaona uhitaji umekuwa ni mkubwa zaidi ya hivi tunavyofanya sisi," alisema Minja.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot