TCRA wazitoza faini milioni 649/- kampuni za simu sita - MUANGALIZI

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Wednesday, July 6, 2016

TCRA wazitoza faini milioni 649/- kampuni za simu sita


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa tume ya mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA James Kilaba
Na Mtumwa Ally

 MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepiga faini ya sh.milioni 649 kampuni sita zinazotoa
huduma ya mawasiliano ya simu za mikononi kwa kukiuka masharti ya usajili wa laini na matumizi yake.

 Makampuni hayo yanadaiwa kukiuka Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (EPOCA) ya
mwaka 2010 pamoja na Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta za leseni za mwaka 2011.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana
kuhusu uamuzi wao kwa makampuni hayo baada ya kukiuka masharti ya usajili wa namba na laini za simu.
Alisema matumizi mabaya ya laini na namba za simu za mkononi, kunahatarisha usalama wa Taifa,
kuchochea tabia hatarishi katika jamii pamoja na kuendeleza matukio ya uhalifu nchini.

Makampuni yaliyotozwa faini hiyo ni Airtel sh. milioni 74 kwa kuruhusu kuuzwa laini 148 bila mnunuzi
kutumia kitambulisho halisi, sh. milioni 33,500 kwa kuruhusu laini 67 ziuzwe bila kujaza fomu za usajili.
Pia kampuni hiyo inatakiwa kulipa faini ya sh. milioni 32,500, kuruhusu laini 65 ziwashwe kabla ya kuuzwa,
sh. milioni 42,500 kuruhusu laini 85 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika katika mtandao.

Kampuni ya Benson Informatics Limited (Smart), imetozwa faini ya sh. milioni 7, kwa kuruhusu kuuzwa
laini 14 bila kitambulisho halisi cha mnunuzi, sh. milioni 7, kuruhusu laini 14 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili
na sh. milioni 3, kuruhusu laini 6 ziwashwe kabla ya kuuzwa.

Nyingine kampuni ya Mic Tanzania Limited (Tigo)
, iliyotozwa faini sh. milioni 93,500, kuruhusu laini 187kuuzwa bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi na sh. milioni 43,500, kuruhusu laini 87 ziuzwe bilakujaza fomu ya usajili.Pia kampuni hiyo inatakiwa kulipa sh. milioni 41, kuruhusu laini 82 ziwashwe kabla ya kuuzwa na sh. milioni 11 kwa kuruhusu laini 22 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao.

Kampuni ya Halotel inatakiwa kulipa sh. milioni 36,500 kwa kuruhusu kuuzwa laini 73 bila kutumia
kitambulisho halisi cha mnunuzi, sh. milioni 36, kuruhusu laini 72 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili na sh.
milioni 34,500 kwa kuruhusu laini 69 ziwashwe kabla ya kuuzwa.

Vodacom Tanzania Limited inatakiwa kulipa sh. milioni 49, kuruhusu laini 98 ziuzwe bila kutumia kitambulisho halisi, sh. milioni 24,kuruhusu laini 48 ziuzwe bila kujaza fomu za usajili, sh. milioni 19 kwa kuruhusu laini 38 ziwashwe kabla ya kuuzwa na sh. milioni 4,500, kuruhusu laini 9 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika katika mtandao.

Kampuni ya Zantel inatakiwa kulipa sh. milioni 36,500 kwa kuruhusu kuuzwa laini 73 bila kutumia
kitambulisho halisi cha munuzi, sh.milioni 11,500, kuruhusu laini 23 ziuzwe bila kujaza fomu za usajili,
sh. milioni 7 kwa kuruhusu laini 14 ziwashwe kabla ya kuuzwa na sh. milioni 2, kuruhusu laini 4 zifanyiwe
usajili wa awali, kutumika mtandaoni.

"Faini hizi zinapaswa kulipwa ifikapo Julai 30, mwaka huu, kampuni zote zimetakiwa kuwasilisha TCRA
orodha iliyohakikiwa ya wakala wa kusambaza na kuuza laini za simu nchi nzima kama inavyotakiwa na
kifungu 92(2) cha EPOCA ifikapo Julai 15 mwaka huu.

"Pia wametakiwa kuacha mara moja kuwatumia wakala, wasambazaji wasioruhusiwa kuuza au kusambaza laini za simu nchini, kuhakikisha laini za simu zinauzwa na wakala anayetambuliwa na mtoa huduma ambaye ana anwani ya makazi inayofikika, mwenye namba tambulishi ya mlipa kodi," alisema.

Mhandisi Kilaba aliongeza kuwa, kampuni hizo zinapaswa kuzima laini zote sokoni ambazo zimewashwa na
kuwasilisha taarifa ya utekelezwaji TCRA ndani ya siku saba kuanzia jana ambapo mtoa huduma ambaye
atakaidi amri hiyo, atachukuliwa hatua kali za kisheria pamoja na kushtakiwa kwa makosa ya jinai.

Alisema ni kosa kutumia namba ya simu isiyosajiliwa ambapo adhabu yake ni faini ya sh. 500,000 au kifungo cha miezi mitatu jela, pia ni kosa kusajili laini kwa kutumia majina yasiyo sahihi.

Aliongeza kuwa, sababu ya kuanzisha utaratibu wa kusajili namba za simu ni kuwalinda watumiaji na jamii kutokana na matumizi mabaya ya huduma za mawasiliano, kuimarisha usalama wa Taifa, kuwa na taarifa ya
matumizi ya simu za mkononi kwa ajili ya maendeleo ya sekta.

Sababu nyingine ni kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano kuwafahamu vizuri wateja wao na
kuwahudumia ipasavyo kadri ya mahitaji yao, kuwatambua watumiaji huduma za ziada za simu kama benki,
kutuma na kupokea fedha, kufanya malipo mbalimbali kwa kutumia simu ikiwemo kulipia huduma ya maji,
umeme.

"Aprili 2013, TCRA na kampuni za simu tulikubaliana juu ya hatua za kumaliza kasoro zilizokuwa
zimejitokeza katika usajili wa namba za simu, pia tulikubaliana kutowezesha laini na namba za simu kutumika kabla ya usajili kukamilika nataarifa za mteja kuhakikiwa," alisema

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot