Mkuu wa Mkoa wa Dar E s Salaam, Paul Makonda.Picha na Maktaba |
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amepiga marufuku uvutaji wa sigara hadharani na kutoa siku saba kwa mahoteli yote yanayotoa huduma za uvutaji wa shisha kusitisha mara moja huduma hiyo.
Makonda alitoa kauli hiyo Dar es Salaam juzi wakati akiwahutubia mamia ya Vijana walioshiriki katika tamasha la Vijana lililoandaliwa na Upendo Media kutoka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Alisema hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote ambaye ataonekana akivuta sigara hadharani kwani suala hilo limekuwa kero kwa jamii ambayo haitumii kitu hicho na kuwafanya vijana kushindwa kufanya kazi.
Alisema ni lazima vijana wafanye kazi na kumtumikia Mungu ili kuwa na Taifa lenye kumcha Mungu kwa kuwa Vijana wengi wanavuta sigara hadharia huku wakijua kuwa wengine hawapendezwi na kitendo hicho.
"Natoa siku saba kwa mahoteli yote yanayotoa huduma za uvutaji wa Shisha kuacha mara moja lakini pia watu wote wanaovuta sigara hadharani kuacha mara moja kufanya hivyo kwani watakamatwa"alisema Makonda
Makonda aliitaka pia Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuwahakikisha kuwa inashughulikia watu wote wanaotumia mitandao ya kijamii kujitangaza kuwa wapenzi wa jinsia moja na (MASHOGA) na wale wanaowaunga mkono.
"Siri ya mafanikio ipo kwa Mungu kwani mimi natoka familia ya kimasikini sana na sikuwahi kufikiria kuwa siku moja nitakuwa RC lakini siri kubwa ni kwamba nilikuwa na hofu ya Mungu"alisema Makonda
Aidha Makonda aliwapongeza Upendo Media kwa kuandaa tamasha hilo la Vijana lilowakutanisha mamia ya vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini wakiwemo waimbaji wa kwaya na wawakilishi kutoka Serikalini ikiwemo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Kanisa la KKKT Mchungaji Ernest Kadiva alisema dhumuni la tamasha hilo ni kuwaleta Vijana pamoja ili kumwimbia Mungu na kufundishwa maadili ya mema yanayompendeza Mungu
"Tunaowamba Vijana kuwa na hofu ya Mungu na kumfuta Yesu ili kuwa watu wema katika jamii"alisema Kadiva.
No comments:
Post a Comment