Chuo cha Dar Es Salaam |
Na Mwandishi Wetu
WALIMU ,wanafunzi na wafanyakazi wa Taasisi za elimu ya juu nchini wameungana kwa pamoja kulaani vitendo vya utoaji na uombaji wa rushwa ya ngono vyuoni ,sehemu za kazi na katika jamii.
Tamko hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa umoja wa kupambana na rushwa ya ngono ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM)Colman Msoka baada ya kumaliza mafunzo juu ya kupinga vitendo vya rushwa ya ngono vyuoni.
Alisema kuwa rushwa ya ngono vyuoni na sehemu za kazi ni tatizo kubwa hapa nchini ikiwa ni pamoja na nyumbani shuleni hata kwenye mikusanyiko mbalimbali ya mikutano ya dini na ya kisiasa.
Pia vitendo vya rushwa ya ngono vyuoni hutokea baina ya wanafunzi na walimu au wanafunzi kwa wanafunzi na waajiri katika sehemu ya kazi.
"Baada ya kupata mafunzo juu ya kupinga vitendo vya rushwa ya ngono katika taasisi ya elimu ya juu yaliyotolewa na taasisi ya mafunzo ya mafunzo ya jinsia(GTI) kwa kushirikiana na Women Fund Tanzania, tunalaani vikali vitendo vya utoaji ngono na uombaji wa rushwa ya ngono vyuoni na katika jamii,"alisema Msoka.
Aliongeza kuwa vitendo hivyo vimekuwa sii vya kibinadamu vimekuwa vinadhalilisha, kunyanyasa na kuondoa ubindamu na tahamani ya utu wake na huchangia kwa kiwango kikubwa kuathirika kisaikolojia.
Pia alisema rushwa ya ngono imekuwa ikisababisha magonjwa, vifo, mifarakano, kulipiza visasi, watumishi hewa, wataalamu wabovu, utendaji kazi duni, nidhamu mbovu miongoni mwa waajiri, wanafunzi na makundi mengine ya watu wanaojihusisha na suala la kuomba na kutoa rushwa ya ngono ili kufanikisha azma zao.
"Kushamiri kwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono kunatokana na imani iliyopo kwa baadhi ya wanawake na wanaume kuwa mafanikio yao yatapatikana kwa urahisi zaidi kwa kutoa rushwa ya ngono,"alisema Msoka.
Alitoa rai kwa viongozi wote wa taasisi za elimu ya juu hapa nchini kuunga mkono juhudi za kuhakikisha tunamaliza tatizxo hili la uombaji na utoaji rushwa ya ngono vyuoni na sehemu za kazi.
Aliwataka watanzania na jamii ya wapenda haki na wanaopinga vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji mtaunga mkono juhudi hizi za kupinga rushwa ya ngono vyuoni na sehemu nyingine katika ngazi ya familia hadi taifa.
Hata hivyo wamevitaka vyombo vya habari kushiriki katika mapambano haya kwa kuandika na kutangaza matukio ya rushwa ya ngono yanayojitokeza kwa jamii ili kuongeza nguvu na kupata sauti ya pamoja itakayoimarisha ya kulaani vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment