Meya wa Jiji la Dar Es Salaam, Isaya Mwita |
Na Carlos Nichombe
JUKWAA Huru la Wazalendo Tanzania limelaani kitendo cha Meya wa Jiji la Dar es salaam, Isaya
Mwita cha kuwapotosha kwa makusudi wananchi wa Dar es salaam na taifa kwa jumla juu ya agizo
halali lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda la kuchukua taarifa za kaya
kwamba ni batili.
Akitoa tamko la kulaani kitendo hicho kilichofanywa na Meya, kwa waandishi wa habari Dar es salaam jana Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Mkoa wa Dar es salaam, Andrew Kadege, alisema jukwaa limesikitishwa na kuibuka kwa Mwita ambaye badala ya kuunga mkono zoezi hilo au kusaidiana na viongozi wenzake yeye ameibuka na kufanya harakati na siasa za kubeza ubunifu huo.
Alisema kauli hiyo ya kiharakati iliyotolewa na Meya imekuja ambapo hata mmoja wa walezi wa UKAWA,
Edward Lowassa akiwa amekemea na kuonesha kuchoshwa na siasa za kiharakati badala ya zile za maendeleo.
Alisema Jukwaa linakemea vitendo vya namna hiyo ambavyo vinarudisha nyuma jitihada za dhati za serikali ya awamu ya tano na kuchelewesha jitihada za serikali katika kuhakikisha wananchi wake wanajikwamua kiuchumi kwa sababu ya siasa tu.
Alisema katika kuonesha Meya si mtu wa maendeleo na wala hana umakini zaidi ya uharakati Meya
anataka wananchi wasitii agizo hilo kwa sababu halina kibali cha kuwapekua wananchi kwa mujibu wa
sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
"Meya amelaghai umma, sheria aliyoitaja inamaanisha utaratibu wa masuala mbalimbali kunapokuwa kumetendeka makosa mbalimbali ya jinai, ni wapi agizo la Makonda limetamka Jeshi la Polisi
likakague watuhumiwa wa makosa ya Jinai," alihoji.
Alisema ni watuhumiwa pekee wa makosa ya jinai ndio wanaotakiwa kukaguliwa kwa mujibu wa sheria
aliyoitaja Meya na kwamba agizo la Makonda liko wazi na lina lenga kuwatambua wananchi wake katika
kaya ili kuweza kupanga mipango ya kuwahudumia kama ambavyo pia mazoezi kama hayo yameshafanyika
katika miji mikubwa duniani kama vile London, Paris na hata Berlin.
Alisema jukwaa linahoji kuna viongozi wa aina gani ikiwa wanashindwa kujua na kutofautisha kati ya siasa na maendeleo, agizo la Makonda ni halali na halihitaji kibali kwa sababu hilo si suala la kisiasa bali ni maendeleo ya wananchi wenyewe na ni sehemu ya maisha ya kawaida kuchukua taarifa za kaya pia kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao.
Aidha Jukwaa hilo linawafahamisha wananchi wa Dar es salaam na maeneo mengine kwamba duniani kote
maendeleo ya watu huletwa na tafiti hivyo Watanzania wote waunge mkono tafiti zinazofanyika ili kuweza kuleta ustawi wa maendeleo wa jamii yetu.
Kadege, aliwaasa wakazi wa Jiji la Dar es salaam na sehemu nyingine litakakofanyika zoezi kama hilo na mengine kutoa ushirikiano kwani kupanga ni kuchagua na takwimu zinahitajika kwa maendeleo ya wananchi hasa wakati huu ambapo serikali inataka kuanza ugawaji wa sh.milioni 50 kwa kila Kaya zilizoahidiwa wakati wa kampeni.
Hivi karibuni Makonda katika kuhakikisha wananchi wa Mkoa wake wanatambulika ili kufanikisha mipango
mbalimbali ya serikali na baada ya mashauriano na wataalamu wake alitangaza zoezi la kuchukua taarifa za Kaya.
Meya ebu acha kuendeleza tofauti zenu za kisiasa, ni wakati wa kuwatumikia wananchi katika kupiga hatua zaidi kwenye masuala ya maendeleo.
ReplyDelete