Nembo ya Chama cha Wananchi CUF |
JUMUIA ya Vijana ya Chama cha Wananchi (JUVICUF) imesema matamko ya kukurupuka ya Serikali ya awamu ya tano na uteuzi wa makada wa Chama cha Mapinduzi(CCM) katika nafasi mbalimbali za uongozi wakiwemo wakurugenzi hayakubaliki na wanaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa ufafanuzi.
Hayo yalisema Dar es Salaam jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi ya JUVICUF Dahlia Majid wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Hamidu Bobali.
Mbali na hilo lakini pia Jumuia hiyo ilitaka pia madaraka ya Rais yapunguzwe ili kuondokana na mambo mbali ya upendeleo ikiwemo katika uteuzi.
Alisema JUVICUF inasikitishwa na tabia ya Viongozi wa Serikali ya awamu ya tano ya kufanya maamuzi ya mlipuko na yasio na tija kwa wananchi na ikiwa hali hiyo itaendelea basi matatizo makubwa yatatokea
Alisema haiwezekani Rais azuie mikutano ya kisiasa hadi mwaka 2020 huku yeye na Chama chake wakiendelea kujiimarisha kwa kuwateua makada kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
"Siasa ni maisha ya kila siku lakini pia kuisha kwa uchaguzi mmoja ndio mwanzo wa uchaguzi mwingine lakini wapinzani wanazuiwa wao wanafanya na kuendelea kujiimarisha kweli kuna haki hapo "alisema Majid
Alisema kitu cha ajabu zaidi ni pale alipowateuwa makada wa CCM kuwa wakurugenzi ambao pamoja na kuwa ndio maafisa ajira katika Wilaya zao lakini pia wao ndio wanatumiwa na NEC katika usimamizi wa Uchaguzi katika maeneo yao sasa kuna kitu kitakachoeleweka baada ya hapo
"JUVICUF inajiuliza hivi ajira katika Halmashauri na Wilaya hazitakuwa zikitolewa kwa kuzingatia itikadi ya CCM ikiwa Mkuu wa Wilaya,Katibu Tawala na Mkurugenzi wote ni makada wa CCM"alihoji Majid
Majid aliongeza kuwa Mwenyekiti wa Jumuia hiyo tayari alishamuandikia barua Mwenyekiti wa NEC kutoa ufafanuzi juu ya hilo na jinsi ilivyojipanga katika kukabiliana na hali hii kwa kuwa wanaushahidi wa kutosha.
Aidha alisema wengi walioteuliwa ambao ni vijana wanawafahamu vizuri sana uwezo wao wa kiubunifu,kusimamia mambo na kuleta mabadiliko yenye tija kwa wananchi ni mdogo ila ni wazuri katika kufanya kazi za ukada
KUTENGUA
Jumuia hiyo ilishangazwa pia na tabia ya kuteua na kutengua na kuhoji kuwa Rais hana washauri wa kumshauri kabla ya kuwateua au anawateuwa mwenyewe bila kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama
"Wiki hii Hadija Usanga aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Mara lakini hakuruhusiwa kuapa na vyanzo vya taarifa zilidai kuwa alizuiliwa kwa sababu hakuwa mwananchama wa CCM"alisema Majid
Aidha Majidi aliongeza kuwa ni uzembe mkubwa wa kumteua mtu na kisha umwambie aje na vyeti vyake kukaguliwa kwani mtu akitangazwa hadharani anatakiwa kuwa alishakaguliwa na kukidhi vigezo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha wa Jumuia hiyo na Mjumbe wa Baraza Kuu la Chama hicho Bonifasia Mapunda alisema licha ya zuio hilo la mikutano hadi 2020 lakini Polisi hawajahi kutoa tamko lolote juu ya Mkutano wa CCM unaotarajiwa kufanyika siku chache zijazo.
Jumuia hiyo ilimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Dar es Salaam Paul Makonda kutafakari matamko yake ambayo mengine bado hajatekelezwa ikiwemo kuwaondoa ombaomba kabla ya kuanza msako wa nyumba kwa nyumba.
No comments:
Post a Comment