ZITO AITAKA POLISI KUFUATA TARATIBU - MUANGALIZI

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Monday, June 13, 2016

ZITO AITAKA POLISI KUFUATA TARATIBU

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge Kigoma Mjini Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) jijini Dar es salaam kuhusu taratibu zifazofanywa na jeshi la polisi

Na Heriard Mwallow

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge Kigoma Mjini Zitto Kabwe amelitaka jeshi la Polisi nchini  kufuata taratibu za kisheria wakati wanapotaka kuwahoji wanasiasa na kuacha kuwavizia majumbani kwao kwaamri zinazotoka juu.

Zitto alieleza hayo jana Jiji Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya taarifa zalizokuwa zimeenea juzi kwenye vyombo mbalimbali vya habari zikieleza kutojulikana alipo kwa muda wa siku mbili taarifa zikilituhumu jeshi la polisi nchini kujua sehemu alipo.

Alisema kuwa alipata taarifa kutoka kwa vijana wake wa usalama kuwa jeshi la Polisi linampango wa kumkamata kati ya siku ya jumamosi hadi jumapili saa 1 jioni na kuongeza kuwa haliwezi kumkamata kwa kumvizia na asipotaka kukamatwa.

Aliongeza kuwa namba zake za simu zipo na wanazifahamu, ofisini kwake kupo na kunafahamika, wasaidizi wake wapo muda wote ofisini hivyo wangeweza kufikisha taarifa za kumhitaji ili kumpata kwa utaratibu.

Alisema jumanne iliyopita alipigiwa simu na jeshi hilo kuwa wanamuhitaji siku ya jumatano na alienda kuhojiwa na kisha kumwambia arudi siku ya jumatano (kesho) lakini cha ajabu safari hii hawakutumia utaratibu huo jambo linalotishia usalama wa maisha yake na wanasiasa wa vyama vingine vya upinzani.

" Juzi saa 1 kasoro watu wetu wa usalama wa chama walinijusha kuwa natafutwa na jeshi la polisi, saa nne usiku walikwenda nyumbani kwangu kunikamata lakini hawakunikuta, jumanne iliyopita nilipigiwa simu na askari mmoja anayehusika na makosa ya jinai Wambura kuwa walikuwa wananihitaji jumatano, nilienda lakini safari hii najiuliza kwa nini sikupewa taarifa" alisema Zitto.

"Tulichukua hatua za makusudi kuhakikisha hawanikamati kwa kuwa hawakutumia njia sahihi inayotakiwa kutumika, ninawasihi watumie njia sahihi zinanazotakiwa kutumika wanapowahitaji wanasiasa si kutuvizia wikendi" alisisitiza Zitto.

Kiongozi huyo alisema kuwa anafahamu lengo kuu la kutaka kumkamata lilikuwa ni kumfanya asiwepo katika kongamano la kujadili bajeti ililokuwa lifanyike jana na kuahirishwa kutokana na jeshi la polisi kuwatisha wenye ukumbi pamoja na hilo la kutaka kumkamata yeye.

Amesema kuhusiana na jeshi hilo kuzuia kongamano hilo, mpaka sasa Polisi hawajatoa sababu yeyote iliyowafanya kuzuia badala yake waliwatisha wenye ukumbi tu kutoruhusu tukio hilo kufanyika.

Amesema hali ya Demokrasia hapa nchini kwa sasa ni tata, kila siku viongozi wa siasa wanaandamwa ikiwemo kuzuia hata kufanya vikao vya ndani kwenye ofisi za vyama au kuzungumza na wafuasi wao vijiweni kama ilivykuwa imezoeleka hapo awali jambo alilolilaani na kusema Magufuli anaharibu nchi kwa kuleta ubabe na kuminya demokrasia.

"Rais Magufuli sifikiri watangulizi wake walioruhusu kukomaa kwa Demokrasia nchini walikuwa wajinga, demokrasia inaondoa machungu, mtu akiudhika alikuwa anenda mwembe Yanga, Mbagala au mwanza anatapika yote kisha mambo mengine yanaendelea" alisema

"Tumeanza kufahamu kwa nini ziara ya kwanza ya nje Magufuli alikwenda Rwanda, alikwenda kujifunza namna ya kuongoza nchi kidkteta, sasa tunamwambia hii ni Tanzania siyo Rwanda, magufuli watu wanamuogopa kumshauri kwa kuwa amekuwa Mungu mtu, wabunge wa CCM wanamuogopa, CCM wanamuogopa ila sisi hatumuogopi tutasema tu hata kama atatufunga, watakuja wengine wataongea"

"Anatengeneza namna ya yeye peke yake kuwa na sauti kwenye nchi hii, hataki kukosolewa, anataka kujifanya ni Mungu mtu na akimaliza wanasiasa atakuja kwa waandishi wa habari, hivyo ndivyo wanavyofanya watawala wote wa kidkteta duniani kote, waandishi jiandaeni ila hatutakubali hili litokee kwenye nchi hii" aliongeza Zitto.

Aidha alisema ACT Wazalendo wanajiandaa kufungua kesi mahakamani kuomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu sheria namba 5 ya mwaka 1992 inayoruhusu vyama vaya siasa kufanya shughuri zake za kisasi bila kuomba kibali bali kutoa taarifa Polisi ili wapewe ulinzi na kuwapongeza Chadema kwa kufungua kesi kama hiyo mwanza na kuomba vyama vingine pia kufungua ili kesi hizo ziwe nyingi.

Kuhusu kongamano la kujadili bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 alisema kuwa walipoona Bungeni wananyanyaswa, mikutano ya hadhara nayo pia ni shida, waliamua kujipanga kivingine na kutumia makongamano hivyo anawaalika wananchi wote kujitokeza kwa wingi kesho saa 9 alasili kwenye ofisi za chama hicho kuendelea na kongamano hilo.

Zitto alisema hiyo ni haki ya kila mwananchi kujadili bajeti ya serikali iwe ndani ya bunge au nje ya bunge ili serikali ijue hisia za wananchi wake na mitazamo yao.

ATUMA SALAMU CCM

Zitto alituma salamu kwa Chama cha Mapinduzi akiwaomba wakae na Rais Magufuli na kumuonya kuacha kuwasakama viongozi wa vyama vya siasa kutokana na CCM pia kuwa chama cha siasa na kueleza kuwa uwepo wa vyama hivyo ndipo ajenda yake ya kukomesha rushwa na ufisadi itakapotekelezwa.

"Magufuli si Mwenyekiti wa CCM, anaingia kwenye Kamati Kuu kwa cheo chake tu sasa wasimuogope, wakae nae na wamuonye aache mambo ya kutumia jeshi la Polisi kuminya Demokrasia, leo ni Rais kesho atakuwa Rais mwingine" Alifafanua Zitto.

"Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchi yetu hatujawahi kupata majaribio ya watu kupindua serikali iliyopo madarakani kama nchi nyingine wanavyofanya kwa kuwa Demkrasia iliimarishwa, sasa akiendelea kufanya hivi na chama chake wakiendelea kumuogopa ajiandae kuwa Rais wa miaka mitano tu" alimaliza Zitto.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot