Wabunge watakiwa kusaidia makamo mwenyekiti kutekeleza ilani ya CCM - MUANGALIZI

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, June 14, 2016

Wabunge watakiwa kusaidia makamo mwenyekiti kutekeleza ilani ya CCM


WABUNGE,Wawakilishi na Madiwani wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja wameshauriwa kumsaidia kikamilifu Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015/2020 ili wananchi wapate maendeleo endelevu.

Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Angelina Adam Malembeka katika hafla fupi ya kuwapongeza madiwani wa mkoa huo iliyofanyika katika Hoteli ya Nungwi Inn huko Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo pia ilihudhuriwa na madiwani kutoka katika Kata ya Ukonga jijnu Dar es Salaam.

Alisema endapo viongozi hao watafanya kazi kwa ushirikiano kwa lengo la kumsaidia utekelezaji wa Ilani hiyo Dkt. Shein ambaye ni Rais wa Zanzibar wananchi wataweza kunufaika na matunda ya CCM.

Alieleza kwamba Dkt.Shein akiwa ni Rais wa  nchi amebeba majukumu mazito hivyo viongozi hao wanatakiwa wamsaidie kutekeleza ahadi ndogo ndogo alizotoa wakati wa Uchaguzi majimboni kwa lengo la kuongeza hamasa na imani kwa wananchi kuendelea kuiamini CCM na kuichagua tena mwaka 2020.

“Sisi tumechaguliwa na wananchi ili tuweze kuwawakilisha katika vyombo vya kufanya maamuzi, lakini pia ni lazima tujue kwamba tunastahiki kumsaidia Rais wetu kutatua changamoto ambazo zipo ndani ya uwezo wetu majimboni.

Pia naamini kwamba tukishirikiana vyema kwa jambo hili kama tunavyoshirikiana kwa mambo mengine basi hakika Majimbo ya Mkoa wetu katika Uchaguzi mkuu ujao hayatasogelewa wala kuguswa na wapinzani”., alisema Angelina na kusisitiza kuwa umoja ndio chimbuko la maendeleo ya Mkoa huo.

Amewasihi viongozi hao kufanya kazi bila ya kutegeana kwani wananchi wamewachagua kwa kuwaamini ili waweze kutekeleza maendeleo ya jimbo kwa haraka zaidi.

Alifahamisha kwamba viongozi hao wasipotekeleza wajibu wao kikamilifu, ipo siku wananchi watawasuta na kujenga hoja za kuwakataa kutokana na kutotekeleza wajibu wao kisiasa ndani ya majimbo yao.

Hata hivyo Malembeka alitoa sh.mil.1 kwa ajili ya kusaidia kufungua akaunti ya kusaidiana katika changamoto mbalimbali ambayo iliungwa mkono na madiwani wa Kaskazini Unguja kwa kuchangia sh.laki 2.

Akitoa mada ya athari ya usaliti ndani CCM, Kada wa Chama hicho kutoka Jimbo la Ilala Dar es salaam, Hassan Kingalu Majole alisema usaliti ndiyo chanzo cha kustawi kwa upinzani Tanzania.

Alisema wafuasi wa chama hicho,wanatakiwa kuweka mbele ukada na misimamo ya kweli ya kuitumikia CCM badala ya kujali maslahi binafsi.

“Wana CCM tuache tabia ya kususa kwani ndani ya chama chetu kuna taratibu zake, na unapokosa nafasi leo we vumilia kesho utapata lakini unapokuwa  msaliti na kutoa nje siri na mikakati ya chama chako jua athari yake haitoishia hapo na itaendelea kutafuna mpaka kizazi chako.”, alifafanua Kingalu.

Akitoa nasaha zake kada wa chama hicho , Batuli Mbaraka aliwasihi viongozi wa CCM nchini kufanya maandalizi mapema hasa kuwa karibu na wananchi ambao ni mtaji halali wa kisiasa na wapiga kura wa CCM kabla ya Uchaguzi mkuu ujao.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya madiwani wa Mkoa huo, Diwani wa Wadi ya Kijibweni Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja, Omar Khamis Abdallah aliwataka viongozi mbali mbali wa mkoa huo kuiga mfano wa Mbunge wa Viti Maalum  Angelina Malembeka kwani kwa kipindi kifupi ameweza kutatua kero za muda mrefu ndani ya Mkoa huo.

Alisema CCM licha ya kuwa na viongozi waadilifu na wakweli katika kusimamia maslahi ya Chama bado kuna baadhi yao wanakwenda kinyume na miongozo na kanuni za Katiba ya Chama.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot