Bia ya Kilimanjaro Premim Lager imekabidhi hundi ya shilingi Milioni 25 kwa Klabu ya Yanga kwa kufuatia klabu hiyo kuwa mabingwa katika Ligi Kuu msimu wa 2015/16.
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika Jijini Dar es Salaam ya kuipongeza Yanga, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema wao kama wadhamini wamefarajika na ushindi huu ambao ni wa pili mfulululizo.
“Hii imedihirisha wazi kuwa Yanga ni timu bora kwa kuwa hii ni mara ya pili mfululizo na ni mara ya sita tangu tuanze kuidhamini kwa hivyo kwetu ni faraja kwa sababu Kilimanjaro Premium Lager inajivunia kuwekeza sehemu yenye ushindi,” alisema.
Meneja huyo alisema moja ya malengo ya kuwekeza katika mpira ni kufikisha soka katika kille cha mafanikio. “Leo hii tunayo furaha kusema kuwa Yanga imetimiza malengo haya kwa kufikia katika kilele cha mafanikio kutokana na udhamini wetu,” alisema.
Alitoa pongezi kwa wachezaji wote, benchi la ufundi, uongozi wa Yanga na mashabiki kwa ushirikiano kati yao ambao ulizaa ushindi huo na kuwataka wasibweteke bali waongeze juhudi ili klabu hiyo iendelee kupata mafanikio.
“Klabu ya Yanga imetangaza Bia yetu ya Kilimanjaro Premium Lager vizuri ndani na nje ya nchi kutokana na matokeo mazuri,” alisema.
Naye Meneja Masoko wa Klabu ya Yanga, Omar Kaya aliishukuru Kilimanjaro Premium Lager kwa ushirikiano mkubwa katika muda wote wa udhamini.
“Tutakuwa wachoyo wa fadhila tusipowashukuru kwa kuwa mumekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri natupa vifaa kwa wakati, mnalipa mishahara ya wachezaji, mmetununulia basi zuri la kusafiria kwa hivyo lazima turudishe shukrani,” alisema.
No comments:
Post a Comment