WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, jana aliwataka viongozi wa dini nchini kushirikiana na Serikali ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya tatizo la rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma na kukomesha matukio ya uhalifu.
Majaliwa aliyasema hayo wakati akimuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye Ibada ya kuwekwa wakfu, kusimikwa Mhashamu Askofu Flavian Kassala kuwa Askofu mpya Jimbo Katoliki Geita.
Alisema siku zote kumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na asasi mbalimbali yakiwemo madhehebu ya dini ili kuwapatia wananchi huduma za kijamii katika sekta ya afya, elimu, maji, utunzaji wa mazingira, ulinzi na ulasama wa jamii na nchi kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa, Serikali inatambua jitihada kubwa zilizofanywa na madhehebu ya dini hivyo wito wake, viongozi wa dini na waumini washirikiane na Serikali kuboresha huduma za jamii, kulinda amani na utulivu, kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
Majaliwa alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa, wajibu wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ambayo yatawasaidia Mtanzania kujikomboa na umaskini, kazi ya viongozi wa dini ni kuunganisha jamii, kukemea waumini wao wasijihusisha na vitendo viovu.
Sisi tunasema kuwa, ushauri wa Majaliwa una maana kubwa kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla kwani maendeleo ya Taifa lolote duniani, hutegemea ushirikiano uliopo kati ya Serikali na wananchi wake katika kudumisha ulinzi, usalama wa Taifa ili kubaini, kuzuia uhalifu.
Ushirikiano unaopaswa kutolewa na jamii ili kuwabaini wahalifu utasaidia kukomesha vitendo vya uhalifu katika makazi hivyo ni wajibu wa jamii kutoa taarifa za wahalifu ili waweze kukamatwa
kupitia doria, operesheni na misako katika maeneo mbalimbali.
Suala la kuzuia uhalifu na wahalifu hutegemea mipango, mikakati na mifumo ikiwemo ya kijamii na kisheria ambao uhusisha vyombo vya ulinzi na usalama, wananchi na kampuni binafsi za ulinzi.
Katika mifumo hiyo, mmoja unaposhindwa kutimiza wajibu wake, husababisha mfumo mwingine kuelemewa na mzigo ambao ungeweza kudhibitiwa kwa urahisi kama mfumo huo ungetimiza wajibu wake wa kubaini na kuzuia uhalifu.
Ni wazi kuwa, wahalifu hawatoki mbali na maeneo tunayoishi bali wapo ndani ya jamii yetu, familia zetu na wengine tunashirikiana nao katika mambo mbalimbali ya kijamii kama misiba, sherehe, michezo, mikutano hata katika biashara.
Wajibu wa kuzuia na kutokomeza uhalifu na wahalifu ni wetu sote ukihitaji nguvu ya pamoja. Kiongozi wa dini ana fursa kubwa kama mlezi wa jamii kuhakikisha waumini anaowaongoza na familia zao, wanaepuka kushiriki vitendo vya uhalifu ambavyo ni dhambi kwa mujibu wa imani.
Imani yetu ni kwamba, miongoni mwa sababu kubwa inayochangia ongezeko la vitendo vya uhalifu na wahalifu ni ukosefu wa malezi bora ndani ya jamii kuanzia ngazi ya familia.
Kama jamii itaendelea kuwa na huruma ya kuwaonea haya wahalifu, malezi hayo hayawezi kukomesha uhalifu badala yake tutafungua mwanya wa ongezeko la matukio ya mauaji na ujambazi.
Ni vyema wananchi wakafahamu kuwa, wajibu wa kubaini, kutanzua na kuzuia uhalifu ni jukumu la kila mmoja linalohitaji ushirikiano kuanzia ngazi ya familia ambazo zinapaswa kujenga malezi bora ya watoto ili watoto wao wasijiingize katika vitendo vya uhalifu.
No comments:
Post a Comment