Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa |
Na: Veronica Kazimoto
Ofisi ya
Taifa ya takwimu imesema kuwa Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Mei, 2016
umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 5.2 kutoka asilimia 5.1 ilivyokuwa
mwezi Aprili, 2016.
Hii
inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka
ulioishia mwezi Mei, 2016 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo
kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2016.
Kwa
mujibu wa wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt.
Albina Chuwa iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam, kuongezeka kwa Mfumuko wa
Bei wa mwezi Mei, 2016 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa
za vyakula na zisizo za vyakula.
Baadhi
ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na
mahindi kwa asilimia 1.5, unga wa muhogo kwa asilimia 6.2, nyama ya kuku kwa
asilimia 2.6, njegere kwa asilimia 5.8, mihogo mibichi kwa asilimia 8.0 na
ndizi za kupika kwa asilimia 2.7.
Bidhaa
zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na
mafuta ya taa kwa asilimia 2.9, mkaa kwa asilimia 2.5, dizeli kwa asilimia 4.6,
petroli kwa asilimia 2.5 na vifaa vya michezo kwa asilimia 7.8.
Taarifa
hiyo imefafanua kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2016 unaopimwa kwa kipimo cha
mwezi umebaki kuwa asilimia 0.5 kama ilivyokuwa mwezi Aprili, 2016. Aidha,
Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 103.00 mwezi Mei, 2016 kutoka 102.46 mwezi
Aprili, 2016.
Aidha,
ulinganifu wa Mfumuko wa Bei kwa baadhi ya nchi za Jumuia ya Afrika
Mashariki, taarifa hiyo inaonyesha kuwa Mfumuko wa Bei nchini Uganda kwa mwezi
Mei, 2016 umeongezeka hadi kufikia asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.1 kwa
mwezi Aprili, 2016.
Kwa
upande wa Kenya, Mfumuko wa Bei umepungua hadi kufikia asilimia 5.00 kwa
mwezi Mei, 2016 kutoka asilimia 5.27 iliyorekodiwa mwezi Aprili, 2016.
Mfumuko
wa Bei wa Taifa kwa kipimo cha mwaka unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya
bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.
No comments:
Post a Comment