![]() |
| Kocha Mkuu wa Yanga, Hans-van-der-Pluijm |
Na Mwandishi Wetu
WAPINZANI wa Yanga katika Kombe la Shirikisho la Afrika, Medeama wametoa onyo kwa Yanga kuelekea mchezo wa marudiano utakaofanyika Jumatano nchini Ghana.
Mkwara huo umekuja baada ya Medeama kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu nchini humo dhidi ya Liberty Professionals huku wakionesha kandanda safi.
Ushindi huo umeongeza ari ya kikosi hicho katika mchezo huo wa marudiano utakaopigwa Jumatano kwenye Uwanja wa Essipong Sports mjini Sekondi-Takoradi. Katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na kuzidi kuiweka Yanga katika wakati mgumu wa kufuzu hatua ya nusu fainali.
Ushindi wa Medeama umeibeba timu hiyo hadi katika nafasi ya tatu ya msimamo huku ikibaki na mchezo mmoja mkononi. Timu hiyo imepoteza mechi moja tu kwenye Uwanja wa Tarkwa na Aboso Park, ikishinda mabao 13 na kutoka sare mara mbili.
Bao hilo pekee lilifungwa na mtaalamu wa mipira ya adhabu, Kwesi Donsu aliyefunga bao lake la saba kwa adhabu kutoka umbali wa meta 25.
Wapinzani hao wa Yanga wana imani ya kusonga mbele baada ya kupoteza mchezo mmojana kutoka sare mbili katika mzunguko wa kwanza hatua ya makundi na hivyo, wakiwa na pointi mbili, huku Yanga ikishika mkia kwa pointi moja, TP Mazembe na Mo Bejaia zikiongoza.
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans-van-der-Pluijm aliiambia Blogu hii jana kuwa, ni lazima wacheze kwa kujitoa ili kupata matokeo mazuri.
“Tunahitaji kuwa wa kipekee kwa kucheza mchezo wa pasi nyingi. Tunajisikia huru tukiamini kuwa tunaweza kubadilisha matokeo,” alisema.
Pluijm alisema wachezaji wake ndio watakaoamua kupata matokeo mazuri iwapo watacheza kwa moyo wa kujitolea. Alisema kila mmoja anapaswa kuamini hilo kwani lolote linaweza kutokea huku akisisitiza kuwa bado wapo kwenye mbio za kuwania kufuzu hatua ya nusu fainali kama tu watajitahidi kushinda mchezo huo.
Kikosi cha wachezaji 30 wa Yanga kilitarajiwa kuondoka leo saa 10 alfajiri kwenda Ghana, tayari kwa mchezo huo wa marudiano, ambapo kati ya hao 21 ni wachezaji na tisa na viongozi.
Meneja wa Yanga, Hafidh Salehe alisema wachezaji wanne wataukosa mchezo huo, akiwemo beki Vicent Bossou mwenye kadi mbili za njano, Hassan Kessy ambaye hajamalizana na klabu yake ya zamani ya Simba, na majeruhi ni Deus Kaseke na Geofrey Mwashiuya.
Kundi A linaongozwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yenye pointi saba ikifuatiwa na Mo Bejaia ya Algeria yenye pointi tano huku Medeama ikiwa ya tatu kwa kujikusanyia pointi mbili na Yanga inashika mkia ikiwa na pointi moja tu hadi sasa.
Mchezo wa Yanga utafanyika kuanzia saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki huku TP Mazembe wakicheza na Bejaia nchini Congo siku hiyo hiyo katika mchezo utakaoanza mapema.



No comments:
Post a Comment