| Mwenyekiti mstaafu Jakaya Kikwete, akimkabidhi vitendea kazi mwenyekiti mpya wa chama hicho Dkt. John Pombe Magufuli katika ukumbi wa chama hicho jana.Picha Na Francis Michael |
BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shinyanga mjini wamempongeza Mwenyekiti mpya wa taifa wa chama hicho, Dkt. John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuendelea kufanya kazi chini ya sekretarieti aliyoirithi ikiongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
Wakizungumza na Blogu hiii kwa nyakati tofauti jana mjini Shinyanga wana CCM hao walisema uamuzi wa Dkt. Magufuli kuendelea na sekretarieti iliyokuwepo utamwezesha kukijenga na kukiimarisha chama kutokana na uzoefu mkubwa alionao katibu mkuu wake Kinana.
Walisema iwapo Dkt. Magufuli angeteua timu mpya ya sekretarieti angekuwa na kazi kubwa katika kukijenga chama kwa vile sehemu kubwa ya wajumbe ambao angewateua wangelazimika kukaa chini na kujifunza kwanza jinsi ya kukiendesha chama hicho hasa ikizingatiwa ndicho kinachoongoza serikali.
“Ukweli mwenyekiti wetu mpya ametumia busara na hekima kubwa kumuomba ndugu yetu Kinana (Abdulrahman) pamoja na sekretarieti yake yote waendelee na nafasi zao, ni uamuzi unaostahili kuungwa mkono na kupongezwa na una faida kubwa kwa mstakabali wa nchi yetu,”
“Iwapo angeamua kuachana na timu hiyo ya Kinana ni wazi angeingiza watu wapya kabisa ambao kwanza ingebidi wakisome chama na ndipo wajue wapi pa kuanzia katika kukiimarisha chama ili kiendane na kasi aliyonayo mwenyekiti wetu mpya wa Taifa, tunamuunga mkono kwa uamuzi huo,” alieleza Rashid Abdalah.
| Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi aliyemaliza muda wake na kurudishwa tena kwenye nafasi yake,Abdullarahman Kinana |
Abdalah alisema pamoja na viongozi waliomo ndani ya CCM kuwa na uzoefu katika masuala ya kichama, lakini kwa kasi na mabadiliko ya uendeshaji wa serikali ya awamu ya tano unaooneshwa na Dkt. Magufuli kwa sasa lazima pia apate timu makini ndani ya chama itakayoweza kumsaidia kikamilifu.
Mwanachama mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Shabani Ramadhani, alisema kasi na utendaji kazi ulioneshwa na Dkt. Magufuli ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake ndani ya serikali ameonesha dhamira ya dhati ya kufanya mabadiliko makubwa ambayo huko nyuma pia Kinana alikuwa akiishauri serikali kuondoa watendaji ‘mizigo’ wanaokwamisha maendeleo ya wananchi.
“Kinachotekelezwa hivi sasa na Dkt. Magufuli, ndiyo kilekile kilichokuwa kikishauriwa na kupigiwa kelele mara nyingi na Kinana katika ziara zake alizokuwa akizifanya katika maeneo mengi nchini, aliwahi kumshauri Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwaondoa mawaziri mizigo ndani ya serikali yake,”
“Kwa misimamo ya Kinana akiunganisha na kasi hii ya Dkt. Magufuli tano ambaye juzi kakabidhiwa rasmi ‘kijiti’ cha uenyekiti wa Taifa wa CCM, ni wazi timu imekamilika, na itakuwa na matokeo mazuri kutokana na watendaji wakuu wake ndani ya Chama na ndani ya serikali kuwa na misimamo inayofanana,” alieleza Ramadhani.
Wanachama hao wametoa wito kwa wana CCM wote nchini na watendaji wa ndani ya chama kuanzia wilaya, mkoa hadi taifa wamuunge mkono mwenyekiti mpya wa Taifa ili aweze kutimiza adhima yake ya kuwaletea watanzania maendeleo ya kweli na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati na ya viwanda.


No comments:
Post a Comment