![]() |
| Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Mkuranga Kunje Ngombale Mwiru(Katikati) akiwa na wadau wa tasnia ya Filamu nchini. |
Aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Mkuranga kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, Kunje Ngombale Mwiru amekitaka chama cha Mapinduzi(CCM) kutoyumbishwa na wapinzani wanaofanya Siasa za maigizo pamoja na kuwataka wapinzani wote nchini kufanya mambo yatakayojenga vyama vyao.
Aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na Gazeti hili kuhusu mkutano wa CCM unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni Dodoma.
Alisema kuwa endapo vyama vya upinzani vitaendelea kushindana na CCM kwa mambo yasiyo na tija vitapelekea kuchokwa na wananchi mapema hivyo kufanya kupotea kwa vyama hivyo ambavyo vinaonekana kuwa ni chachu ya mabadiliko katika Taifa.
Aliongeza kuwa wapinzani wanatakiwa kuacha tabia ya kukurupuka na kuanzisha mijadala mbali mbali nchi ambayo imekuwa haina faida na badala yake wajikite katika kuanzisha mambo yatakayoigwa na chama hicho kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.
"Ukiangalia hivi karibuni Vijana wa Chadema walitishia kuzuia mkutano mkuu wa CCM, binafsi naona hizo ni ndoto za mchana na kujitafutia umaarufu usiokuwa na faida katika mabadiliko wanayosema na tunafahamu kwamba watanzania hawahitaji siasa za maigizo bali wanahitaji wanasiasa wachapakazi," alisema Kunje.
Akizungumzia uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, Kunje alisema kuwa wanasiasa wa vyama vya upinzani wanapaswa kuiga mfano toka CCM kwani wamekuwa na utaratibu wa kupishana kuongoza vyama vyao tofauti na ilivyo kwa vyama vyao.
Alisema kuwa Vyama vya upinzani viache tabia ya kuwapokea maveterani wa siasa kutoka CCM na kuwapeleka katika kugombea nafasi za uenyekiti wa Kikanda umekuwa ndio mwanzo wa kuua vyama vya upinzani nchini.
Pia alisema kuwa wapo baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wamekuwa wakisema serikali ya awamu ya tano imekuwa ikikandamiza vyama vya upinzani na kusema kusema kuwa wamekuwa wakijikandamiza wenyewe kutokana na mambo wayafanyayo yasiyo na manufaa kwa chama na jamii.



No comments:
Post a Comment