![]() |
| WAZIRI wa Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Jenista Mhagama |
Na Heriard Mwallow
WAZIRI wa Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Jenista Mhagama amelitaka Baraza la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi kuratibu, kusimamia, kufuatilia na kutathimini masuala yote ya uwezeshaji ili Watanzania waweze kushiriki kwenye masuala ya uwekezaji hapa nchini.
Kutokana na majukumu hayo kuwa ndiyo msingi wa uanzishwaji wa Baraza hilo ameliagiaza pia kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji na tathimini utakao iwezesha Serikali kupata taarifa za ushiriki wa Watanzania kwenye nyanja za ajira, manunuzi na ujengaji uwezo.
Mhagama alitoa maagizo hayo jana Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa mashauriano ya ushiriki wa Watanzania katika uwezseshaji ulioshirikisha wadau mbalimbali wa uwekezaji hapa nchini.
Aidha aliwaagiza wadau mbalimbali kutoka sekta zote za umma na binafsi kuhakikisha zinatoa ushirikiano kwa Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kufanikisha kazi hiyo kwa mstakabali wa nchi yetu.
Mhagama aliziagiza pia taasisi zilizopewa barua za kuteua waratibu wa ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji wahakikishe wanateua waratibu hao haraka iwezekanavyo ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huu mhimu wa ushiriki mhimu wa Watanzania katika uwekezaji.
Alisisitiza kuwepo kwa ushirikiano mzuri kati taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi ili kupitia ushirikiano huo mpango huo uweze kufanikiwa na kuleta manufaa kwa Taifa.
Alisema Tanzania ni moja ya nchi duniani zilizobahatika kuwa na rasilimali nyingi zinazohitaji kusimamiwa ipasavyo ili ziweze kunufaisha Watanzania walio wengi na kwa kutambua hilo Srikali imeweka mikakati madhubuti ya kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye uchumi
"Dhana ya ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji ni dhana mpya hapa nchini inayohitaji kufahamika kwa wadau wengi kwa kuwa kwa kuwa ni nguzo mhimu katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji" alisema Mhagama.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Beng'i Issa alisema kuwa takwimu za miaka ya hivi karibuni zianaonyesha pato la Taifa limefikia Dola za Kimarekani bilioni 46.87 kwa mwaka na kueleza kuwa pato hilo litaongezeka zaidi kutokana na uwekezaji uliofikiwa kwenye sekta za Nishati, Madini na Gesi Asilia.
Vilele kutokana na jitihada za Serikali za kuweka mazingira mazuri yanayovutia ni wazi kutakuwa na ongezeko zaidi la wawezeshaji katika sekta za kiuchumi kama vile Ujenzi, Uchukuzi, Mawasiliano, Maliasili, Kilimo, Viwanda, Mifugo, Uvuvi na biashara.



No comments:
Post a Comment