WAKALA wa uchimbaji visima na Ujenzi wa mabwawa(DDCA) umesema kuwa ufinyu wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya kazi zao umepelekea wakala huo kutengeneza majengo yasiyo na viwango vinavyohitajika.
Pia umesema kuwa kuwepo kwa wataalamu wasio na viwango katika makampuni binafsi yanayojihusisha na shughuli hiyo hapa nchini umepelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la mabwawa yasiyo na uwezo wa kuzalisha maji.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam jana Mkuu wa kitengo cha masoko na uhusiano wa wakala huo, Nungu Egwaga alisema kuwa uchimbaji wa visima pamoja na mabwawa umekuwa ukitumia gharama nyingi lakini kutokana na kutokutengwa kwa fedha ya kutosha kumepelekea miradi mingi kujengwa kwa kiwango cha chini.
Alisema kuwa kabla ya kuanza ujenzi wa mabwawa pamoja na visima hapa nchini wamekua wakifanya tafiti mbalimbali zikiwemo zile za kufanya uchunguzi wa udongo pamoja na kupima ubora ya mabomba ambayo yatatumika kupitisha maji toka kwenye eneo mabwawa yalipo kwenda kwa wananchi, hivyo kukosekana kwa fedha za kutosha kumepelekea kuruka baadhi ya hatua ambazo zilitakiwa kufuatwa.
Aliongeza kuwa kutokana na ujenzi wa mabwawa na visima kuhitaji gharama kubwa wamekua wakiomba mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha lakini wamekua wakikataliwa kupewa mikopo hiyo kwa kuwa wakala ni taasisi ya serikali hivyo hawawezi kukopeshwa na taasisi hizo za kifedha.
"Tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali za kupata mikopo toka sehemu mbalimbali ikiwemo mabenki lakini majibu tunayoambiwa ni kwamba hatuwezi kukopeshwa fedha kwakuwa sisi tupo chini ya serikali, na hii miradi inagharimu fedha nyingi na serikali inauwezo wa kugharamia visima na mabwawa machecho kwa mwaka kitendo kinachotupelekea kuchimba na kujenga visima pamoja na mabwawa machache" alisema Nungu.
Hata hivyo aliongeza kuwa wakala utaendelea kuwashawishi taasisi za fedha kukubali kuwakopesha fedha kwa kutumia miradi wanayoijenga kama dhamana ya mkopo huo, na kufanya hivyo kutapelekea kuongeza kasi ya ujenzi wa mabwawa pamoja na visima hapa nchini.
Nungu alisisitiza kuwa wataendelea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na taasisi mbali mbali zinazohitaji kujenga mabwawa pamoja na visima kutumia mifumo ya maji ya matanki ambayo gharama zake zimekuwa sio kubwa ukilinganisha na ule wa mabwawa.



No comments:
Post a Comment