![]() |
| mchele |
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS)limeteketeza tani mbili za mchele wa Pakistani zilizokamatwa katika bandari ya Dar es Salaam ukiwa unatokeo Zanzibar.
Akizungumza wakati wa uteketezaji wa bidhaa hizo jijini Dar es salaam jana, Ofisa udhibiti ubora wa TBS, Grangay Masala alisema mchele huo ulikamatwa May 12 mwaka huu bandari ya Dar es Salaam ukitokea Zanzibar.
Alisema baada ya kukamata Mchele huo ambao ulikuwa tani 6 wenye thamani ya sh. milioni 10 walienda kupima katika maabara ya TBS na kugundua kuwa tani mbili zimeshaisha muda wake wa matumizi.
Alisema mchele huo umetokea Pakistani kupitia bandari ya Zanzibar hivyo kutokana na muda wake wa matumizi kwisha unaweza kuleta madhara kwa watumiaji.
"TBS imepima mchele huo katika maabara zake na kujiridhisha kuwa mchele huo haufai kwa matumizi ya binadamu hivyo tunateketeza kuepusha madhara kwa wananchi,"alisema Masala.
Alisema mchele huo endapo ungetumika unaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu kama kupata fangasi wanaotengeneza sumu mwilini, kansa ya ini na kudumaa kwa watoto.
Kwa upande wake Ofisa husiano wa (TBS)Neema Mtevu, amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanaingiza bidhaa zenye ubora na wawe walinzi tosha wa kuhakikisha bidhaa hafifu haziingizwi nchini.
Pia alisema kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kufuata taratibu za nchi katika uingizaji wa bidhaa na kuepuka kuingiza bidhaa zilizo chini ya kiwango.
Alisema TBS wapo kila eneo kuhakikisha wanadhibiti bidhaa zilizo chini ya kiwango kuhakikisha haziingii nchini.



No comments:
Post a Comment