RAHCO kuvunja Nyumba pembezoni mwa reli - MUANGALIZI

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, June 21, 2016

RAHCO kuvunja Nyumba pembezoni mwa reli

Moja kati ya nyumba zilizopo pembezoni mwa Reli ya kati zinazotakiwa kubomolewa

Na Rose Itono

UONGOZI wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) umesema jukumu la kuondoa majengo yaliyopo kandokando ya Reli hiyo ni ya  Kampuni Hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO).

Kaimu Mkurugenzi wa TRL Masanja Kadogosa aliyasema hayo Dar es Salaam hivi karibuni baada ya kuulizwa swali na waandishi wa habari waliotaka kufahamu hatma ya baadhi ya maghorofa na majengo mengine yaliyoko kandokando ya reli kinyume cha sheria.

Kadogosa kabla ya kujibu swali hilo alikiri kuwepo kwa baadhi ya majengo kandokando ya reli likiwemo lile ghorofa lililopo eneo la gerezani karibu kabisa na reli ya kati kwa kusema kuwa, jukumu la kuondoa majengo hayo lipo mikononi mwa Rahco. 

Akizungumzia muingiliano wa kikazi uliopo baina ya TRL na RAHCO ambapo hivi karibuni wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliitaka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania kuiacha TRL ijiendeshe yenyewe alisema kuwa, suala hilo tayari liko mikononi mwa serikali.

"Ni kweli kuna muingiliano wa majukumu ya kikazi baina ya  TRL na RAHCO lakini kwa kuwa tayari wabunge wameliongelea bungeni, nina imani suala hilo litashughulikiwa kwani tayari lipo mikononi kwa serikali",aliongeza Kadogosa. 

Aidha aliwataka wananchi pamoja na wadau wa reli  kuwa na subira wakati suala hilo likifanyiwa kazi lengo ni kuhakikisha miundombinu ya reli inalindwa.

Hata hivyo hivi karibuni TRL ilianzisha msako maalumu kuwabaini wabadhirifu wa miundombinu ya reli baada ya kupata taarifa kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakichota kokoto zinazosambazwa kwenye njia ya reli ili kupunguza vumbi wakati treni linapita na kwenda kuziuza kwa wajenzi bila kujali ni gharama kiasi gani inatumika na serikali kuboresha miundombinu ya reli.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot