| Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa Nape Nnauye |
Na Carlos Nichombe
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amewataka Viongozi wa soka nchini kuchangamkia na kusimamia fursa mbali mbali za michezo zitokeazo ili kuweza kukuza tasnia huyo.
Aliyasema hayo jana Dar Es Salaam alipokuwa akizindua msimu wa 6 wa michezo ya 'Airtel Rising Stars kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, unaodhaminiwa na kampuni ya Airtel.
Alisema kuwa viongozi wa mikoa na Taifa wanatakiwa kusimamia kwa umakini michuano mbali mbali inayo anzishwa hapa nchini kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kuongezeka kwa vijana wenye vipaji ambavyo vitaweza kulisaidia Taifa.
"Tumeona taasisi mbali mbali zimeweza kujitokeza na kuanzisha michezo ya kuibua vipaji hivyo kama viongozi wetu wataweza kuungana na taasisi hizi kwa hakika hali ya michezo katika taifa letu itakuwa iko juu kwa kuwa vipaji vitakuwa vimeibuliwa vingi na viongozi wetu watakuwa wamefanikiwa kuvilinda" alisema Nape.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel hapa nchini, Beatrice Singano aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi katika Fursa mbali mbali zitolewazo hapa nchini kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kujitengenezea ajira ambayo itawapatia kupato na kusaidia kukuza uchumi wa nchi.
Alisema kuwa kampuni hiyo imeweza kutoa fursa ya vijana kushiriki katika michezo ya mpira wa miguu kwani wanafahamu kwa kufanya hivyo wanaweza kupunguza matatizo yatokeayo katika jamii kwa kuwa wengi wao watakuwa wakifuatilia mambo ya msingi na kupunguza muda wa kukaa vijiweni na kufanya mambo mabaya.
"Tunafahamu hali iliyopo katika jamii kwa hivi sasa kwahiyo tunaamini kupitia michezo tutaweza kupunguza matukio mabaya ambayo yamekuwa yakitokea na kuhatarisha amani ya nchi yetu, huvyo serikali ituunge mkono ili kuweza kutimiza malengo hayo tuliyojiwekea" Alisema Singano.
Hata hivyo kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini(TFF), Jamal Malinzi amewataka vijana kuwa wawazi wa kutaja umri wao pindi waendapo kufanya usajili wa kujiunga na michezo mbali mbali hapa nchini.
Alisema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kuongopa Umri wao kwa madai ya kuwa Serikali haiwezi kuwabaini watu hao na kusema kuwa kitendo hicho wakifanyacho kimekuwa ni kinyume cha Sheria na kinarudisha nyuma maendeleo ya Soka.
"Vipo vipimo vinavyoweza kufanywa na wataalamu wetu ili kuweza kubaini umri wa mtu alioutaja kama itakuwa ni sahihi au sio sahihi, kwahiyo kama wanapenda kuona nchi yetu inapiga hatua katika soka waache kuongopa umri ili tuweze kuwatumia watu hao katika sehemu itakayokuwa inahitajika kuwatumia ikiwemo katika timu za vijana wale wenye umri chini ya miaka 17 au 20" alisema Malinzi
Michezo ya Airtel Rising Stars msimu wa 6 itashirikisha vijana wa kiume toka mikoa ya Mwanza, Morogoro, Mbeya, Temeke na Ilala pamoja na moikoa ya Ilala, Kinondoni, Temeke, Arusha, Lindi na Zanzibar kwa wasichana.


No comments:
Post a Comment