Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
John Pombe Magufuli amelitaka jeshi la Polisi kutumia mbinu za medani
linapokabiliana na matukio ya uvunjifu wa amani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
kuwa wanawanyanganya majambazi silaha kabla ya kutekeleza uhalifu wowote.
Rais Magufuli amesema hayo wakati wa uzinduzi wa
kituo cha mawasiliano cha Jeshi la Polisi ambacho kitarahisisha utoaji wa
taarifa za uhalifu na kuharakisha askari polisi kufika katika eneo la tukio.
Kituo hicho cha kwanza kuanzishwa na Jeshi la
Polisi hapa nchini kipo katika kituo kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es
salaam na kinafanya kazi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu na mfumo
wa utambuzi wa eneo (GPS) ambapo askari polisi waliopo katika kituo cha
mawasiliano watakuwa wakipokea simu kutoka kwa wananchi wanaotoa taarifa za
matukio ya uhalifu na kisha kuwaelekeza askari walio jirani ili wafike eneo la
tukio na kukabiliana na wahalifu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali
(IGP) Ernest Mangu amemueleza Rais Magufuli kuwa kituo hicho kina uwezo wa
kupokea simu 18 kwa mpigo kutoka kwa watu wanaopiga simu ya bure namba 111 au
112 kwa ajili ya kutoa taarifa za uhalifu na kwamba lengo la jeshi hilo ni
kuhakikisha askari wanafika eneo la tukio ndani ya dakika 15.
IGP Mangu ameongeza kuwa kituo hicho kimeanzishwa
kwa msaada kutoka benki ya CRDB iliyotoa shilingi milioni 320, kitaanza kutoa
huduma tarehe 01 Julai, 2016 kikianzia katika mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni
Kanda maalum ya Dar es salaam na polisi imejiwekea malengo ya kuwa na vituo
kama hivyo nchi nzima ifikapo mwaka 2019.
Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho, Rais
Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuanzisha mradi huo na ameahidi kuwa
serikali itahakikisha inaunga mkono mpango huo ikiwa ni pamoja na kulifanyia
kazi ombi la kununuliwa helkopta itakayorahisisha zaidi ufikaji eneo la tukio.
Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi
kuwanyang’anya silaha wahalifu kabla hawajawadhuru raia na kupora mali zao ama
kusababisha mauaji, na amewataka viongozi wa jeshi hilo kuwazawadia askari
wanaofanya kazi nzuri ya kupambana na wahalifu.
Dkt. Magufuli pia ametaka jeshi la polisi
lisimame imara kuhakikisha serikali inatekeleza ahadi zake kwa wananchi
zikiwemo upatikanaji wa maji na huduma nyingine za kijamii na kwamba hatarajii
kuona mtu yeyote anafanya vitendo vitakavyosababisha ahadi hizo kutotekelezwa.
| Rais Magufuli akiangalia kituo kipya cha mawasiliano jijini dar es salaam |



No comments:
Post a Comment