Na Grace Ndossa
HALMASHAURI zote nchini zimetakiwa kuhakikisha zinatenga fedha asilimia 10 za vijana na wanawake kutoka kwenye mapato ya ndani kama walivyoagizwa.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene alipokuwa akizindua Tawi jipya la Benjamin Mkapa city la Benki ya Biashara ya (DCB).
Alisema kuwa Halmashauri pamoja na kutenga fedha hizo bado ni ndogo kwani asilimia 10 haijafika hivyo lazima wafanye hivyo kama walivyoagizwa.
"Fedha zilizotolewa na Ilala milioni 700 kwa ajili ya vijana na wanawake na fedha zilizotolewa na Wilaya ya Kinondoni milioni 997 siamini kama ndo asilimia kumi ya mapato ya ndani hivyo bado wanatakiwa kutekeleza agizo hilo,"alisema Simbachawene.
Hata hivyo aliipongeza benki ya DCB kwa kujitahidi kupiga hatua na kutoa gawio kwa wanahisa pamoja na mtaji wao kuongezeka kutoka bilioni 1.1 tangu mwaka 2002 hadi kufikia bilioni 32.
Alisema halmashauri zote zinatakiwa kukaa na kukubalina waweze kuweka fedha zao huko kama walivyokubaliana awali kuanzishwa kwa benki hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Edimund Mkwawa alisema Benki imeweza kupata faida na kutoa gawio kwa wanahisa kwa kipindi cha miaka kumi mfululizo ambapo kwa mwaka 2015 bilioni 11.73 zimetolewa kama gawio ikilinganishwa na sh milioni 215.4 zilizotolewa mwaka 2006
Alisema benki hiyo inatoa bilioni 1.55kama gawio kwa wanahisa wake kwa faida ya mwaka 2015 ambapo ametoa hundi kwa baadhi ya wanahisa.
"Mtaji wa benki umeongezeka kupitia uuzaji hisa za haki na hisa za awali kupitia soko la hisa la Dar es salaam ambapo DCB imekuwa benki ya kwanza nchini kujiunga na soko hilo Novemba 2008,"alisema Mkwawa.
Hata hivyo alisema kuwa DCB imekuwa ikipata faida tangu mwaka 2004 ambapo faida ilikuwa milioni 447.6 na kwa mwaka 2015 faida baada ya kodi imefikia bilioni 3.1
Alisema kuwa tawi walilozindua ni la tisa kwa hapa Dar es Salaam na wanaendelea kuboresha na kusogeza huduma za kibenki karibu na wananchi .
Pia DCB inatoa sehemu ya faida inayopatikana kusaidia jamii inayoizunguka na kwa mwaka huu tunatoa madawati 300 yenye thamani ya sh milioni 39 kwa shule za msingi Mkoa wa Dar es Salaam ili kukabiliana na uhaba wa madawati.
Mwisho


No comments:
Post a Comment