Mhandiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitillya Mkumbuko akizungumza na wadau wa elimu katika moja ya mikutano ya hakielimu |
BALOZI wa Sweden Nchini Tanzania Katrina Rangnitt amezindua mpango mkakati wa miaka mitano 2017/2021 wa Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Haki Elimu unaojikita katika uboreshaji elimu nchini Tanzania.
Akizindua mpango huo balozi wa Sweden Rangnitt kwa kushirikiana na bodi ya taasisi hiyo, alisema kuwa mkakati huo ni kufanya ushawishi kwa serikali ili iandae na kutekeleza sera ambazo zitakuwa fursa kwa watoto hususani katika kuandikishwa shule, usawa wa elimu jumuishi iliyo bora, inayotolewa kwenye mazingira rafiki na salama kwa wote.
Pia alisema mkakati huo utahakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa, wanajipanga kwa kushiriki katika kutatua changamoto zilizopo katika shule nyingi nchini hususani kwa kufuatilia utawala na utoaji elimu bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Haki Elimu John Kalage, alisema kuwa mkakati huu wa miaka mitano ni kuhakikisha wanashawishi mabadiliko ya sera na utekelezaji wake.
Alisema elimu ya Tanzania haina falsafa iliyo wazi hivyo inashindwa kufiki ujumuishaji kamili wa makundi yote na kutoa matokeo bora ya kujifunza yenye manufaa kwa wanafunzi.
"Shule si sehemu salama kwani mtoto mmoja kati ya wawili hukumbana na ukatili ambao umezoeleka kutendwa na walimu hivyo kuna haja ya kufanya marekebisho zaidi sera ya elimu na kampeni ya kuhimiza utekelezaji makini wa sera ya elimu ya mwaka 2014 ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu na ubora wake vinaimarika,"alisema Kallage.
Alisema licha ya juhudi za serikali zinazoendelea, sekta ya elimu nchini Tanzania bado imesongwa na changamoto kubwa ambazo ni pamoja na matokeo duni ya ufundishaji wa wanafunzi, utoro wa Waalimu na uwezo mdogo wa kufundisha na kukosekana kwa usawa wa kijinsia.
Pia alisema kushamiri kwa mfumo tabaka wa elimu ni tatizo kwani watoto wa wenye fedha wachache wanapata elimu bora kwenye shule binafsi na masikini wanaachwa kwenye elimu duni katika shule za serikali.
Aliongeza kuwa kukosekana kwa falsafa na malengo ya elimu vinavyoeleweka kwa kila mtu matokeo yake, elimu ya Tanzania imekosa falsafa na malengo ya kuiongoza.
Naye Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam Profesa Kitillya Mkumbo,alisema serikali inatakiwa kuchukua hatua za muda mfupi za kutatua changamoto za elimu ya msingi kutokana na mfumo ambao siyo bora.
Pia alisema Mtazamo wa serikali kwa vyuo vya ufundi bado msukumo wake ni mdogo, hivyo wanatakiwa kuelekeza nguvu katika vyuo hivyo ili kupata watu wenye ujuzi na kufikia lengo la kuwa na serikali ya viwanda.
Vile vile alisema elimu ya juu hapa nchini inawalimu wachache wenye shahada ya uzamivu ambapo ni asilimia 25 tu na chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndiyo wenye walimu wengi wenye shahada hizo hivyo kuna haja ya serikali kuwekeza kwenye elimu na kutoa elimu bora.
No comments:
Post a Comment