DC MKURANGA AWATAKA MADEREVA BODABODA KUZINGATIA SHERIA - MUANGALIZI

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Monday, December 19, 2016

DC MKURANGA AWATAKA MADEREVA BODABODA KUZINGATIA SHERIA

 Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Wilaya ya Mkuranga Albert Sanga amewataka madereva bodaboda wa wilaya hiyo
kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani pindi waendeshapo vyombo vyao vya moto ili kuweza
kupunguza tatizo la ajari katika wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Albarto Sanga akizungumza na madereva bodaboda wakati wa hafla fupi ya kuwakabidhi vyeti pamoja na leseni zao.

Hayo aliyasema juzi wilayani humo wakati alipokuwa akizungumza na madereva hao wakati wa sherehe za
kuwatunuku leseni na vyeti madereva bodaboda zaidi ya 1580 waliohudhuria mafunzo ya uendeshaji wa vyombo vya moto.

Akizungumza na madereva hao katika hafla hiyo, Sanga aliushukuru uongozi wa chuo cha New Vision kwa kutoa mafunzo bora ya udereva kwa madereva wa bodaboda wa wilaya hiyo na kuongeza kuwa mafunzo hayo yataweza kuleta maendeleo kwa madereva hao na kuongeza hali ya uwajibikaji ambayo kipindi cha nyuma walikuwa hawana.

Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega akiwaelekeza jambo madereva wa bodaboda wilaya ya Mkuranga, katika hafla hiyo Ulega alitoa kiasi cha Sh. Milioni moja ili kuweza kufanikisha malengo ya chama hicho cha bodaboda
Alisema endapo madereva hao wataweza kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani wataweza kupunguza ajari za mara kwa mara na kuongeza uzalishaji wa malighafi mbalimbali zitakazoweza kuiinua wilaya hiyo kiuchumi.

"Lakini pamoja na kuzingatia sheria za usalama barabarani nawaomba sajilini chama chenu na kama mtaweza kufanya hivyo basi mtakuwa mmefungua fursa mbalimbali ikiwemo za kupata mikopo itakayowanufaisha katika mambo yenu ya udereva wa bodaboda pamoja na hali ya maisha kiujumla," alisema Sanga.

Aliongeza kuwa madereva hao wanapaswa kuongeza bidii katika kufanya kazi zao ili waweze kununua pikipiki zao wenyewe badala ya kutrgemea pikipiki za watu wengine ambazo zinawafanya wasipate mafanikio.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chuo cha Udereva cha New Vision, Jonas Bigoya alisema tatizo la ajari za barabarani linaweza likaepukika endapo madereva wataweza kuhudhuria mafunzo mbalimbali katika vyuo vilivyosajiliwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema Watanzania wanapaswa kutambua madereva bodaboda na wao wanafanya kazi kama wafanyavyo watu wengine katika sekta muhimu za kukuza uchumi wa nchi hivyo kutoa mafunzo kwao kutaweza kuwaongezea ujuzi na mbinu mbalimbali za kuweza kuboresha mazingira yao ya kazi.

"Chuo chetu tumegundua tatizo la ajari kwa jinsi linavyozidi kutokea hapa nchini na tutaendelea kutoa elimu maeneo yote ya nchi ili tuweze kutoa elimu na kutokomeza tatizo la ajari linalozidi kutokea mara kwa mara," alisema Bigoya.

Bigoya alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Pwani kukiruhusu chuo hicho kupita katika kata zote za mkoa huo ili kuweza kutoa elimu kwa wananchi ambao wanamiliki vyombo vya moto.

Aliongeza chuo hicho kitaweza kutoa mafunzo hayo ya udereva kwa gharama nafuu ambazo zitamuwezesha kila mtanzania kumudu gharama hizo tofauti na baadhi ya vyuo ambavyo vimekuwa vikitoza gharama kubwa zinazowafanya watanzania wengi kushindwa kuhudhuria masomo hayo.








Mkaguzi msaidizi wa Polisi Mkuu Usalama barabarani Mkuranga, Hamidu Mtiginjole akiwaasa madereva wa bodaboda wilaya ya Mkuranga kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani pindi watumiapo vyombo vya moto.
Akizungumza kwa niaba ya Wanakikundi cha Timu Safiri na Safari Salama inayoundwa na wanachama zaidi ya kumi, Mwenyekiti wa kikundi hicho Edward Chienela alisema kuwa waliamua kuaandaa programu hiyo pasipo malipo ili kuweza kutoa elimu kwa wananchi wanaoshindwa kwenda mjini kupata elimu ya udereva.

Alisema kikundi hicho kitaendelea kuandaa programu za aina hiyo ili kuweza kuhakikisha madereva wote wa wilaya hiyo wanaendesha vyombo vyao hali ya kuwa wanaelimu ya kutosha.

Mafunzo hayo yaliyotolewa kwa muda wa mwezi mmoja yaliweza kuhudhuriwa na madereva zaidi ya 1580 kutoka katika kata 25 za wilaya hiyo huku 1407,wakitunukiwa vyeti, 600 wakitunukiwa leseni zao na 807 wakiwa wanasubiria mchakato wa kukamilisha leseni zao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot