![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, Picha na Maktaba. |
Akizungumza na wadau mbalimbali waliojitokeza katika uzinduzi wa zoezi la uchangiaji wa damu lililoandaliwa na Jumuiya ya Akhlaaqul Islam (JAI) katika viwanja vya Mwembe Yanga Jijini Dar es Salaam, Lyaniva amesema kuwa watanzania wanapaswa kujitokeza kwa wingi katika kushiriki kazi zinazoonekana kuokoa uhai wa wananchi ikiwemo zoezi hilo muhimu la uchangiaji damu.
Amesema kwa sasa kumekuwa na uhitaji mkubwa wa damu katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na makundi yanayohitaji damu kuwa mengi zaidi na kuongeza kuwa endapo watanzania watajitokeza kwa wingi katika uchangiaji wa damu wataweza kupunguza tatizo hilo ambalo linaonekana kugharimu maisha ya wagonjwa wengi.
Lyaniva amesema kitendo cha kujitolea kuchangia damu ni cha kiungwana na kinapaswa kutendwa na kila mtu mwenye vigezo vya kufanya hivyo kwani damu hainunuliwi madukani kama ilivyo bidhaa nyinginezo ambazo zinatengenezwa kiwandani.
Hata hivyo Lyaniva amewataka madereva wanaotumia vyombo vya moto kuendesha pole pole vyombo hivyo na kueleza kuwa endapo watakuwa wakiendesha kwa kufuata taratibu za usalama barabarani wataweza kupunguza ajari za mara kwa mara na kupelekea mahitaji ya damu kuwa madogo tofauti na ilivyo sasa ambapo ajari zimekuwa zikijitokeza kila kuchapo.
"Nadhani mnatambua kwamba damu inapatikana kwa binadamu pekee na kujitolea kutoa damu yako kwa watu usiowajua kwa hakika unapata swawabu kubwa kutoka kwa Mungu kwa sababu damu hii inakwenda kuokoa maisha ya maelfu ya watanzania wenye uhitaji wa damu kila siku wakiwemo Majeruhi wa ajari, Watoto, Wamama wajawazito pamoja na wagonjwa wa Saratani ambao wote kwa ujumla wanawategemea ninyi," alisema Lyaniva.
Kwa Upande wake Mlezi wa JAI, Sheikh Nurdin Kishki amewataka waislamu kushindana katika kufanya mambo mema yenye lengo la kulisaidia taifa katika utatuzi wa matizo mbalimbali yanayolikabili badala ya kushindana kufanya mambo yanayovunja umoja na mshikamano ambayo yanapelekea kuvunjika kwa amani ya taifa.
![]() |
Sheikh Nurdin Kishki, Picha na Maktaba. |
Amesema waislamu wanapaswa kushindana katika matukio muhimu ya shughuli za kijamii kunawafanya wazidi kupata heshima katika taifa la Tanzania na kuongeza kuwa endapo wataendelea kubishana na kushindana katika masuala ya vita jamii ya watanzania haitawaamini na itawaona kama vile ni watu wasio na maana yoyote ile.
"Nataka mtambue hata katika vitabu vyetu vitakatifu vimeonesha umuhimu uliopo katika kushiriki shughuli hizi za kijamii na leo hii natarajia kuona misikiti ikishindana katika kuleta waumini wao kuja kutoa damu kwa sababu nahakika hiki kitendo ni cha kiungwana kuliko vyote tuvitendavyo," alisema Kishki.
Ameongeza kuwa katika zoezi hilo la ukusanyaji wa damu wanatarajia kupata chupa zaidi ya Elfu tatu ambazo zitakabidhiwa kwa damu salama ili kuweza kuzigawanya kwenye hospitali zenye uhitaji wa damu.
No comments:
Post a Comment