WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali imeviagiza vyombo vya dola hapa nchini kuhakikisha vinawadhibiti madereva wazembe wanaotembea ovyo barabarani na kusababisha ajali za kizembe mara kwa mara.
Majaliwa alitoa kauli hiyo Jijini Dar es salaam jana wakati alipokuwa akitoa salamu za Sikuu ya Idd El Fitri katika Swala ya Idd iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema kuwa ajali iliyohusisha mabasi mawili ya Kampuni moja ya City Boys iliyotokea huko Singida na kuua watu 30 sio ya kawaida bali ni tukio lililofanywa na madereva kwa uzembe wao wenyewe.
" Sisi kama serikali tumeviagiza vyombo vya dola kuhakikisha wanadhibiti madereva wanaotembea ovyo na kuvunja sheria za usalama barabarani lengo likiwa ni kudhibiti ajali za kukusudia kama hii," alisema.
Katika kuadhimisha sikukuu hiyo, Majaliwa aliwataka waislamu wote hapa nchini kujihifadhi vyema kama walivyoweza kuishi katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Alisema kama waislamu wameweza kuishi vyema na kuepuka kutenda maovu katika kipindi chote cha mwezi mtukufu waendelee kufanya katika siku zote za maisha yao ikiwemo katika siku hizi za sikukuu na kuongeza kuwa waislamu wanapaswa kusherehekea sikukuu hiyo kwa amani na kuacha kufanya mambo yatakayovunja amani.
Aliwasisitizia waislamu kuacha tabia ya ulevi, wizi na vitendo vya dhuluma kama walivyofanya katika kipindi chote cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Aliwapongeza waislamu kwa kutimiza moja ya nguzo za dini yao ya kufunga iliyoagizwa na Mtume na kuwataka waweze kufunga siku sita zijazo kwani kwa kufanya hivyo wataweza kujitwalia baraka zote.
Aliwataka waumini wa dini hiyo kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake kwani hali iliyopo hivi sasa inahitaji viongozi washupavu na jasili hivyo kwa maombi yao viongozi hao wataweza kusimamia vyema nchi.
Naye, Mufti Mkuu wa Tanzania, shekhe Abubakary Zubeiry, aliwasisitizia waislamu kudumisha umoja na amani miongoni mwa jamii na kuacha kuendeleza tabia za uhasama.
Alisema hakuna haja ya kushikilia tofauti za kidini kwani maendeleo ya Taifa na Jamii kwa ujumla yanaletwa kwa ushirikiano wa pande zote bila kujali dini, rangi wala kabila.
"Nawaomba waislamu wote wakati tunasherehekea siku hii muhimu kuhakikisha kwamba tunaondoa tofauti zetu za kidini pamoja na kikabila kwani vitu hivi vilianzishwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi," alisema.
Shekhe Mkuu wa Mkoa Wa Dar Es Salaam, Alhadi Mussa Salum |
Kwa upande wake Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam. Alhadi Mussa Salum, alisema waislamu wanapaswa kuadhimisha siku hiyo kwa amani na utulivu na kuacha vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Alisema ni vyema waislamu wakatumia siku hii muhimu kusherehekea pamoja na familia zao na kuacha kutenda mambo yaliyo kinyume na matakwa ya Mungu.
Pia aliwataka Waislamu Kote nchini kutumia siku ya siku kuu ya idd kwa kuwatembelea na kuwasaidia Yatima, Wajane Na Maskini ili na wao waweze kupata faraja kutoka kwa waumini wa dini hiyo.
"Zipo siku kuu nyingi ulimwenguni lakini Siku kuu hii ni muhimu sana kwa waumini wa kiislamu kusherehekea na familia zetu na niwatake kuitumia siku hii kwa kuwasamehe wote waliowakosea na kuimarisha udugu uliopotea kwa kipindi kirefu, pia pamoja na hayo yote tunapaswa kuitumia siku hii katika kuwasaidia na kuwatembelea wale wote wenye uhitaji ili kuweza kuongeza faraja kwa wote ili waweze kutambua umuhimu wa siku hii adhimu," alisema.
No comments:
Post a Comment