![]() |
| Baadhi ya simu bandia zilizofungwa |
Na Penina Malundo
SIMU bandia Laki 6 tayari zimezimwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)na kusababisha asilimia 2.6 ya watumiaji wa simu hizo kukosa mawasiliano.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwa njia ya Simu,Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya TCRA, Innocent Mungi alisema simu hizo bandia zimeweza kuleta athari nyingi kwa watumiaji.
Alisema takribani asilimia 3 ya watumiaji wa simu hizo wameweza kuathirika na utumiaji wa simu hizo ambazo zinasababisha maradhi mbalimbali.
Mungi alisema Mchakato wa uzimaji wa simu hizo bandia unaendelea kwani mtambo umewashwa tayari kwa ajili ya kuzima simu hizo hivyo mtu yeyote mwenye simu bandia hata akitoka nje ya nchi na akiingia nchini simu yake itazima.
"Tumewasha tayari mtambo tangu (jana)juzi usiku hivyo simu bandia zote zinakata mawasiliano zenyewe kutokana na namba za IMEI kutooana,tayari simu zenye IMEI tofauti tofauti zimeshazimwa takribani IMEI laki 6,"alisema Mungi
Aidha alisema kuna baadhi ya watu wanaosema kuwa simu zao ni feki na bado hazijazimwa na kuona kuwa zoezi hilo halijafanyika,watumiaji hao wanajidanganya kwani mtambo tayari umewashwa na IMEI nyingi zimeshafungiwa.
"Kutokana na uelewa wa watu kuwa mgumu ndio maana watu wanasema simu zao feki bado hazijazimwa,simu tunazozizima sisi ni zile ambazo IMEI zake hazioani, na kunavigezo ambazo mtambo huo wa uzimaji unaangalia,na kudai kwamba asilimia kubwa ya watu hawana uelewa wa kugundua simu zao feki au sio feki,hali hiyo inapelekea watu kutojua kama simu zao bandia na kubaki kusema simu hazijazimwa jambo ambalo sio la kweli"alisema
Alisema Watanzania wenye simu bandia wahakikishe simu zao wanazipeleka katika makampuni ya simu za mkononi ambazo ndio sehemu pekee zinapokusanyiwa simu hizi bandia kwa sasa.
"Tumetoa tahadhari kuhusu simu hizi bandia ni hatari kwa matumizi ya binadamu kwani yanaleta athari mbalimbali tayari tunashirikiana na Baraza la Mazingira (NEMC) katika kuhakikisha simu hizi zinakusanywa na kuhifadhiwa sehemu husika,"alisema
Mungi alitoa wito kwa watanzania kutumia simu orijino ambazo hazitaweza kuwaletea athari yeyote.
Miongoni mwa watu waliozimiwa simu zao,Janeph John alisema simu yake aina ya KZG ilizimika jana (juzi) usiku kama TCRA ilivyosema.
Alisema ameathirika vibaya na uzimwaji huo wa simu yake kwani alikuwa anaitegemea katika mambo mbalimbali ikiwemo katika matumizi ya biashara zake pamoja na kupoteza mawasiliano na watu wake.
"Najipanga kununua simu mpya sasa naamini itakuwa orijiono,ila kuzimwa kwa simu hizo zimeweza kutuathiri kwa kiasi kikubwa sisi watu wenye hali duni ya maisha,inatubidi tutafute simu orijino ambazo zinauzwa kwa bei kubwa,"alisema
Naye Yona Ezekia alisema kumetokea na athari ya ziada ambapo watu wengi kushindwa kumudu bei za simu orijino ambazo kwa kawaida huwa ziko juu ukiachilia mbali ongezeko la bei litakolotokana na ongezeka la mahitaji ya bidha hiyo.
"Upandaji wa bei wa simu hizi orijino kutawafanya watu wengi kushindwa kununua simu hizo kwa uharaka kufidia pengo litakalokuwa limejitokeza na hivyo kuchukua muda mrefu zaidi kwa hali kurejea katika hali ya kawaida,"alisema Ezekia
Kwa Upande wake Muuzaji wa Simu kutoka Soko la Kariakoo,Athumani Said alisema ni bora zoezi hilo limefanyika ili sasa waanze kuuza simu.
Alisema awali wateja wa simu walipotea kutokana na kuhofia kuuziwa simu bandia hata kama maduka ya simu kwa wakati ule yalikuwa yakiuza simu orijino.
"Ni kweli tumepata hasara kubwa sana lakini tutafanyaje na Serikali ndio imeamua,bora sasa wateja wataanza kujitokeza na kurudisha imani simu zinazouzwa kuwa ni orijino na sio bandia kama walivyofikilia kabla ya zoezi la uzimwaji wa simu bandia,"Alisema
Ameiomba Serikali kudhibiti uingizwaji wa simu feki ambazo zimewasababishia wao kupata hasara nyingi na kuathiri watumiaji wengi wa simu hizo bandia.



No comments:
Post a Comment