![]() |
| Mwenyekiti wa makampuni ya IPP Reginald Mengi |
MWENYEKITI wa makampuni ya IPP, Dkt. Reginald Mengi ametoa msaada wa madawati 1000 yenye thamani ya Sh milioni 70 kwa Halmashauri za Wilaya ya Bagamoyo na Handeni.
Fedha hizo zimegawanyishwa katika wilaya hizo mbili huku kila moja ikipata mgao wa Sh. milioni 35 na kila dawati likitengewa Sh. elfu 70.
Msaada huo ni moja ya juhudi za serikali za kupambana na upungufu wa madawati hapa nchini huku lengo likiwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu kusiwe na mwanafunzi anayekaa chini.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Dkt. Mengi alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakipuuza kutoa msaada katika mambo ya elimu wakidhani wanaofaidika ni wanaopata elimu pamoja na wazani wao jambo ambalo si kweli.
Alisema, mtu anapojitoa na kusaidia elimu unasaidia jamii nzima kwani ndani ya hao wanafunzi ndimo wanapopatikana madaktari, walimu pamoja na watu wengine wanaotoa huduma mbalimbali na kusaidia jamii.
Alisema kuwa ni wazi kuwa mtu anapojitoa na kusaidia elimu basi anasaidia Taifa zima katika kupambana na kuondokana na umaskini kwani miaka ya mbeleni hakutakuwa na mwanafunzi atakayelalamika kwa kukosa elimu bora.
"Endapo wadau na watu wenye uwezo tukijitoa kwa pamoja kutatua tatizo hili nina imani kuwa tutalimaliza kabla hata ya kufikia mwisho wa mwezi huu", alisema Dkt. Mengi.
Alisema, watu wenye uwezo hasa wafanyabiashara wanatakiwa kukumbuka watu wa hali ya chini na kuchangia shughuli za kielimu kwani watu hao ndio wamekuwa wanunuzi wakubwa wa bidhaa zao na wao kupata faida kubwa.
Aidha aliwapongeZa wakuu wa wilaya hizo kwa jitihada kubwa wanazozifanya kuhakikisha suala hili linamalizika kabla ya muda kama alivyoagiza mkuu wa nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Husna Rajab alisema kuwa wilaya yake ilikuwa na upungufu wa madawati 7552 lakini kutokana nna kupata msaada wa madawati 4000 hadi sasa upungufu uliopo ni wa madawati 3000.
Alisema kuwa msaada uliotolewa na dk. Mengi ni mkubwa sana kwani utasaidia kupunguza idadi ya madawati yanayohitajika.
"Tunashukuru sana kwa kupata msaada huu na tunaamini itakuwa chachu ya kukuza na kuongeza ufaulu katika Wilaya yetu na siku moja kushika nafasi za juu katika ufaulu wa nchi", alisema Bi. Raraja.
Naye mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majjid Mwanga alisema kuwa wilaya yake yenye jumla ya shule za sekondari 25 na msingi zaidi ya mia moja ilikuwa na upungufu wa jumla ya madawati 10353.
Alisema kuwa baada ya Rais, Dkt John Pombe Magufuli kutoa agizo hilo kila kata za Bagamoyo na Chalinze zilitakiwa kuchangia madawati 50 huku kila kijiji kikipewa agizo la kuchangia madawati 380 na uongozi wake.
Alisema kutoka na utekelezaji wa agizo hilo hadi sasa madawati 4350 yapo katika hatua za mwisho.
Alhaj Majjid alisema kuwa mbali na madawati pia walikusanya sh. milioni 36 kutoka kwa wadau mbalimbali huku pia Sh. milioni 13 zikikusanywa kutoka kwa madiwani na wakuu wa idara mbalimbali.
Alisema hadi sasa wilaya yake imeshafanikiwa kukusanya jumla ya madawati 7890 na upungufu uliobakia ni wa madawati 2463.
"Madawati yaliyobakia si mengi sana ila tutafanikiwa kufikia malengo endapo watajitokewa watu wenye moyo wa utu na kusaidia wengine kama alivyofanya Dkt. Mengi na ni imani yetu hadi kufikia mwishoni mwa mwezi tutakuwa tumepunguza upungufu huo", alisema Alhaj Majjid.



No comments:
Post a Comment