- MUANGALIZI

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, June 21, 2016

Mkurugenzi wa Sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA),Onorius Njole(kushoto) akizungumza na waandishi wa habari

Na Carlos Nichombe

Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii - SSRA imesema kuwa imejizatiti kupanua wigo na kuboresha huduma ya hifadhi za jamii hasa kwa kundi lililo katika sekta isiyo rasmi.

Hayo yalisemwa jana Dar es salaam na Mkurugenzi mkuu wa Huduma za sheria wa mamlaka hiyo, Onorius Njole alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mpango wao wa kuanza kuunganisha wafanyakazi walio katika sekta zisizo rasmi.

Alisema kumekuwa na uhitaji mkubwa wa watu walio katika ajira ndogo ndogo kuweza kujiunga na mifuko mbali mbali ya hifadhi za kijamii lakini kutokana na taratibu mbali mbali zilizopo ziliwakwamisha watu hao kuweza kujiunga na mifuko hiyo.

"Mwaka jana tuliweza kufanya utafiti katika sekta ya Usafiri pamoja na nyinginezo na tumefanikiwa kugundua asilimia 83 ya watu ambao wapo katika mfumo usio rasmi wanataka kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa hiyo walishindwa kujiunga kutokana na mifumo kutokuwatambua watu wa aina hiyo" alisema Njole.

Hata hivyo Njole alisema kuwa moja kati ya majukumu ya mamlaka hiyo ni kusimamia utendaji kazi wa mifuko yote ya hifadhi ya jamii, hivyo katika kusimamia hilo wameandaa program maalum kwa ajili ya kutoa elimu kwenye mifuko mbali mbali ya hifadhi ya jamii.

Alisema kuwa kwa kuanza mamlaka hiyo itaanza kutoa elimu kwa wakurugenzi wa mamlaka za halmashauri za wilaya pamoja na waratibu wa mifuko ya bima ya afya ya jamii(CHFs) nchini kote kwa kuwa watu hao ndio waendeshaji na wasimamizi wakuu wa CHF katika wilaya zao.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na masuala ya afya, Wizara yenye dhamana ya masuala ya hifadhi ya jamii na SSRA inafanya mapitio ya mfumo wa usimamizi wa mifumo ya Bima ya afya ya jamii kwa lengo la kuja na mfumo utakao weza kutoa huduma ya afya kwa watanzania wote.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot