Katibu wa Yanga, Boniface Mkwasa |
HATIMAYE Uongozi wa Klabu ya Yanga, umefunguka na kusema wapo katika mchakato wa mwisho wa kukamilisha malipo ya deni la aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ernest Brandts aliyevunjiwa mkataba wa kuifundisha timu hiyo miaka miwili iliyopita.
Yanga imetakiwa kulipa dola 11,000 za Marekani kama ambavyo iliamriwa Juni 30, 2015 na Kamati ya Hadhi ya Wachezaji ya FIFA, jambo ambalo lilipuuzwa na klabu hiyo kwa muda mrefu kabla ya FIFA kuibuka na kutishia kuishusha daraja Yanga endapo wasipolipa deni hilo.
Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Charles Mkwasa amesema suala hilo lilikuwa ni la muda mrefu na walikuwa wakilifanyia kazi lakini kutokana na kupewa maagizo kwa uzito mkubwa wameamua kulifanyia kazi kwa haraka ili kulimaliza suala hilo kabla ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA haijakaa kwenye vikao vyake vinavyotarajiwa kukaa siku yoyote.
Amesema Uongozi wa klabu hiyo unatambua kwamba wanadaiwa kiasi hicho cha fedha kilichoelezwa na FIFA wiki iliyopita na kuwataka mashabiki wa klabu hiyo kuondoa hofu ya timu yao kushushwa daraja kwa kuwa uwezo walionao kwa ajili ya kulipa deni hilo ni mkubwa.
"Suala hili tulianza kulijadili toka mwaka 2014 mara baada tu ya kuvunja mkataba na Brandits, lakini kulikuwa na baadhi ya mambo mbalimbali yaliyoingiliana hapa katikati na kukwamisha kutekeleza mpango ambao tulijiwekea,"
"Lakini hata kama FIFA isingetupa hili agizo ni lazima tungelimaliza hili suala haraka kwa sababu tulikuwa tunatambua mchango mkubwa aliouonesha Brandts katika kuhakikisha Yanga inakuwa bora kwa wakati wake ule aliokuwa akiifundisha timu yetu," alisema Mkwasa.
Kitendo cha Yanga kutolipa deni hilo kwa wakati, imetafsiriwa kwamba imevunja Kanuni ya 64 inayozungumzia Nidhamu katika FIFA yaani FDC (FIFA Disciplinary Committee).
Ikumbukwe FIFA iliieleza klabu ya Yanga siku chache zilizopita kama watashindwa kumlipa Brandts fedha zake hizo kabla ya kamati kuketi na kufanya vikao vyake watakua wamekiuka sheria na kanuni mbalimbali za soka na adhabu mbalimbali zinaweza kuwakumba ikiwemo Kukatwa pointi katika michezi ya Ligi ya Vodacom inayoendelea nchini au kushushwa daraja.
Wakati huo huo, Mkwasa amewataka mashabiki wa Yanga kuwa na imani na timu yao inayotarajia kusafiri jumamosi kuelekea nchini Comoro wanakwokwenda kucheza mchezo wa ligi ya mabigwa dhidi ya Ngaya Fc.
Amedai kuwa kocha wa timu hiyo, George Lwandamina kwa ushirikiano na benchi lake la ufundi wataweza kuwatoa kimasomaso mashabiki wa timu hiyo kutokana na wao kama uongozi kuwapatia vitu vyote vya muhimu vinavyohitajika katika mashindano hayo.
Amesema hawezi kuzungumzia zaidi mchezo wao dhidi ya Ngaya kwa kuwa tathmini hiyo inapaswa kutolewa na kocha wa timu hiyo ambaye anatambua uimara na udhaifu wa wachezaji wake wanaounda timu yake.
"Mimi kwa sasa sipendi kusema mchezo huo utakuwa ni mgumu au sio mgumu kwa sababu mimi sipo kwenye benchi la ufundi la Yanga kwa hiyo kazi hiyo tumwachie kocha na benchi lake, lakini kama kiongozi wa Yanga nikiangalia mahitaji tuliyowatimizia hawa wachezaji na makocha wetu basi watafanikiwa tu kwenye mechi zao," aliongeza Mkwasa.
Katika mchezo huo utakaopigwa Februari 12 huko nchini Comoro Klabu ya Yanga itamkosa beki wake, Andrew Vicent 'Dante' kutokana na mchezaji huyo kupata kadi nyekundu katika mchezo wa Kombe la shirikisho uliofanyika mwaka jana dhidi ya Timu ya TP Mazembe ya DR Congo.
No comments:
Post a Comment