Dk Shein awaapisha mawaziri, wakuu wa wilaya - MUANGALIZI

Hot

Post Top Ad

Your Ad Spot

Thursday, March 1, 2018

Dk Shein awaapisha mawaziri, wakuu wa wilaya

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein leo Machi 1, 2018 amewaapisha viongozi aliowateua jana Februari 28, 2018 kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Taarifa iliyotolewa na Ikulu Zanzibar leo, inaeleza kuwa hafla hiyo imefanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Baadhi ya viongozi hao ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd; Spika wa Baraza la Wawakilishi,  Zubeir Ali Maulid; Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu; Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,  Said Hassan Said; mawaziri, naibu mawaziri na wakuu wa mikoa.
Walioapishwa ni Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi, Amina Salum Ali;  Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Ali Abeid Karume; Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji na Dk Sira Ubwa Mamboya.
Wengine ni Waziri wa Afya, Hamad Rashid Mohamed; Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi,  Rashid Ali Juma; Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Salama Aboud Talib; Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo pamoja Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Maudline Cyrus Castico.
Pia wamo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Juma Makungu Juma;  Naibu Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Choum Kombo Khamis; Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Shadia Mohamed Suleiman; Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Dk Makame Ali Ussi na  Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda, Hassan Khamis Hafidh.
Pia, Dk. Shein amewaapisha wakuu wa wilaya aliowateua ambao ni  Issa Juma Ali (Mkoani-Pemba) na Rajab Ali Rajab wa Kaskazini B, Unguja.
Viongozi walioapishwa wameahidi kuendelea kumsaidia Rais Dk. Shein katika kuhakikisha Zanzibar inazidi kupata maendeleo, kuimarisha ushirikiano na kuwatumikia wananchi.
Pia, wameahidi kuleta mabadiliko na kufanya kazi kwa vitendo sambamba na kuendelea kusimamia amani na utulivu uliopo nchini.
Jana, Dk Shein alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mapinduzi kwa kuongeza wizara moja zaidi na kuwabadilisha wizara baadhi ya Mawaziri.
Kufuatia mabadiliko hayo, shughuli za vijana zimehamishiwa katika Wizara mpya ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo shughuli za mazingira zimehamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na shughuli za Wakala wa Serikali wa Uchapaji zimehamishiwa Wizara mpya ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale.
Aidha, amewateua naibu mawaziri wapya wawili na kumbadilisha wizara naibu waziri mmoja ambapo kufuatia mabadiliko hayo, SMZ hivi sasa ina wizara 14.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot