![]() |
| Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa |
Na Mwandishi Wetu,
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amempongeza mdau wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini (SAGCOT) kwa upande wa ufugaji, ASAS Diaries Limited kwa kuwainua wafugaji wadogo wadogo mkoani Iringa.
Akitembelea shamba kubwa la mifugo linalomilikiwa na ASAS jana, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wawekezaji wengine nchini kuiga mfano wa mwekezaji huyo kwani itasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima.
“Huu ni mfano mzuri wa uwekezaji ambao unasaidia wafugaji wadogo wadogo wanaomzunguka mwekezaji mkubwa kunufaika kwa soko la uhakika,utaalam na huduma za kijamii pia,” alisema waziri mkuu.
Majaliwa amejionea ufugaji mkubwa wa kisasa katika shamba hilo ambalo lina ng’ombe wa kisasa wa maziwa zaidi ya 1,000 na kuwataka wafugaji wadogo kuchangamkia fursa wanazozipata.
“Wakati sasa umefika kwa Watanzania kupenda bidhaa zinazotengenezwa hapa nyumbani kwani zipo zenye ubora wa hali ya juu,” alisema waziri mkuu na kuongoza kuwa ameridhishwa na uwekezaji kwenye shamba hilo la mifugo la ASAS.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa ASAS Diaries Limited, Fuad Jaffer, alisema kampuni imefanikiwa katika uboreshaji wa mifugo, udhibiti wa magonjwa ya mifugo kuzalisha mitamba na madume bora.
“Tumefanikiwa kuimarisha mahusiano mazuri na jamii kwani Kampuni imeajiri watumishi wengi kutoka maeneo yanayotuzunguka,” alisema Jaffer.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alimwambia waziri mkuu kuwa kiwanda kinasindika lita 14,000 za maziwa kila siku ambayo ni sawa na asilimia 24 ya uwezo wa kiwanda.
Waziri Mkuu alitembelea shamba hilo la ASAS ambaye pia ni mdau muhimu wa SAGCOT, ikiwa njiani kuelekea katika Mkoa wa Njombe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kongani na Ubia wa Maendeleo wa SAGCOT, Maria Ijumba, aliwaambia waandishi wa habari kuwa ASAS ni mfano wa kuigwa kwa wadau wa SAGCOT kwenye sekta ya ufugaji.
“Kwa kweli Serikali inapaswa imuunge mkono kwa dhati kwani mchango wake katika jamii zinazomzunguka ni mkubwa sana. ASAS mbali ya kuwasaidia wafugaji wadogowadogo anachangia sana katika maendeleo ya jamii zinazomzunguka,” alisema Ijumba.
Ijumba alitoa pia mwito kwa Watanzania kujijengea tabia ya kupenda kunywa maziwa yaliyosindikwa na hasa yalitengenezwa hapa nchini.
“Sisi kama SAGCOT tunafanya kazi kwa karibu na wadau wetu ili wafikie malengo waliyojiwekea,” alisisitiza.



No comments:
Post a Comment