![]() |
| Ni moja kati ya meli zinazoongozwa na maharia wa kitanzania |
MABAHARIA Nchini wameilalamikia mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini(SUMATRA) kuwa ndio kisababisho kikuu cha wao kuweza kukosa Ajira katika kampuni mbali mbali za meli.
Pia wameitaka Serikali kuanzisha kitengo maalum cha ulinzi wa bahari ambacho kitakuwa kikifanya doria majini wakati wote ili kuweza kusaidia kupunguza matukio ya uharamia ambayo yanaonekana kutishia uhai wao.
Hayo yalisemwa jana Dar es salaam na Mkufunzi Mkuu wa Chuo Cha Mabaharia Dar es Salaam(DMI) Kapt. Konsi Mgawe wakati wa maadhimisho ya siku ya mabaharia Duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika chuo hicho.
Kapt. Mgawe alisema vyeti vinavyo tolewa na SUMATRA vimekuwa havitambuliwi kimataifa hivyo kupelekea mabaharia wengi waliosoma Tanzania kukosa kazi pindi wafanyapo maombi ya kazi katika Makampuni hayo ya kimataifa.
"Sekta ya Usafirishaji wa majini ndio kiini kikuu cha ukuaji wa uchumi kwa kuwa sekta zote zinaitegemea sekta hii katika kufanya usafirishaji, hivyo Serikali ione haja ya kuweza kutusaidia mabaharia ili tuweze kwenda kufanikisha suala hili lakini kama tusipo saidiwa hatutoweza kuifanya nchi yetu ikue kiuchumi" alisema Kapt.Mgawe
Kwa upande wake Kaimu mkuu wa Chuo cha DMI, Dkt. Tumaini Gulumo aliitaka Serikali pamoja na wadau wa masuala ya usafiri wa majini Kuwajali mabaharia pamoja na kukipatia vifaa chuo hicho ili kuweza kutoa Elimu itakayo wafanya mabaharia waliopitia katika chuo hicho kuwa Bora.
Alisema Sekta inayopelekea kukuza uchumi kwa kasi ni Sekta ya Bahari kwa kuwa watalii, Mali ghafi zitumikazo kuzalishia mali viwandani pamoja na madawa vyote hutegemea sekta hiyo, na kuitaka serikali kuwekeza zaidi katika sekta hiyo ili kuifanya kuzidi kuwa na tija.
"Asilimia kubwa ya Vitu vitu vyote nchini inategemea Sekta hii kwahiyo lazima Serikali iwekeze zaidi kwenye sekta hii na tutaweza kuinua na kukuza uchumi wa nchi yetu tofauti na ilivyo sasa" alisema Dkt. Tumaini.
Hata Hivyo Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Wira ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani aliyekuwa mgeni rasmi alizitaka SUMATRA pamoja na watendaji wakuu wa wizara yake kuchukua hatua ili kuweza kutatua changamoto hizo zinazowakabili mabaharia hapa nchini.
Aliongeza kuwa kutokuwepo kwa Mamlaka halisi ya Bahari kunaweza kuipeleka nchi kuingia katika mgongano hivyo kuahidi kuweza kufanyia kazi suala hilo ili liweze kumalizika na kuiacha nchi katika hali sahihi.
"Leo nilifika hapa kusikiliza na kujifunza mambo mbali mbali yaisumbuayo sekta hii lakini niwaombe nikitoka hapa nitweza kuzungumza na mamlaka zote zinazohusika na sekta hii ili tuweze kuzimaliza changamoto zinazoikanili sekta hii muhimu" alisema Ngonyani.
Maadhimisho hayo ya siku ya mabaharia duniani yameadhimishwa hapo jana huku mabaharia pamoja na wadau wengi wao kulalamikia changamoto mbali mbali zinazoikabili Sekta hiyo.
Kwa upande wake Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho(DAMISO) George Mnali aliiomba serikali kuwanunulia Meli ya kufanyia mafunzo ili kuongeza hali ujuzi kwa wanafunzi wanaoshiriki katika kozi hiyo.



No comments:
Post a Comment